Mvutano wa mitandaoni kati ya Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, na kiongozi wa upinzani Bobi Wine umechukua sura mpya.
Hii ni baada ya Jenerali Muhoozi, ambaye ni mtoto wa Rais wa muda mrefu wa Uganda, Yoweri Museveni, kutangaza kwenye mtandao wa X kwamba angetaka “kumkata kichwa” Bobi Wine. Katika ujumbe wake wa Jumapili jioni, Muhoozi alidai kwamba baba yake, ambaye ametawala Uganda tangu 1986, ndiye anayemlinda Bobi Wine dhidi yake.
Bobi Wine, ambaye alimaliza wa pili katika uchaguzi wa urais wa 2021 dhidi ya Museveni, alijibu vitisho hivyo akisema kuwa anazichukulia kwa uzito kutokana na historia ya vitisho na mauaji kwa wafuasi wake.
Jenerali Muhoozi hakusita kujibu tena, akimdhihaki Bobi Wine kwa maneno: “Nimekuamsha? Kabla nikumalize kwanza tulipe mkopo tuliokupa,” akionekana kudai kuwa Bobi Wine alihongwa na serikali ya Uganda kupunguza moto wa upinzani.
Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Uganda pamoja na Jenerali Muhoozi hawakupatikana kuelezea kauli hizo, Msemaji wa jeshi naye alikataa kuzungumzia mtafaruku huo.
Bobi Wine amepinga vikali tuhuma hizo, akisisitiza kuwa hajawahi kupokea fedha kutoka kwa serikali. “Kama walinifadhili, kwa nini wananifuatilia kila mahali na kuua wafuasi wangu?” alihoji.
Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, alikuwa mwanamuziki kabla ya kuingia kwenye siasa. Katika uchaguzi wa 2021, alipinga matokeo ya urais akidai udanganyifu na vitisho dhidi ya wapiga kura.