MECHI mbili ambazo Simba imecheza dhidi ya vibonde wa Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika, CS Sfaxien, zimempa faida mara mbili kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids.
CS Sfaxien ni vibonde wa kundi hilo kutokana na hadi sasa kutopata pointi yoyote katika mechi nne za hatua ya makundi ambapo timu zote zimecheza huku vinara wakiwa CS Constantine wenye pointi tisa sawa na Simba, kisha Bravos (6).
Sasa basi, faida ya kwanza Fadlu aliyoipata ni kukusanya pointi sita kutokana na kushinda nyumbani na ugenini dhidi ya CS Sfaxien zilizoifanya Simba kufikisha pointi tisa zinazowasogeza karibu zaidi na kufuzu robo fainali.
Faida ya pili ni kiwango kilichoonyeshwa na kiungo mkabaji wa Waarabu hao, Balla Moussa Conte ambaye amekuwa kivutio kikubwa kwa Fadlu kiasi cha kuhitaji huduma yake huku akimtumia kipa wake, Moussa Camara kumshawishi atue Msimbazi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinabainisha kuwa, mara ya kwanza Fadlu alivutiwa na uwezo wa kiungo huyo katika mchezo uliopigwa hapa Dar Desemba 15, 2024 ambapo Simba ilishinda 2-1 huku Conte akikichafua dakika zote tisini.
“Baada ya mchezo wa kwanza, Fadlu akataka kujidhihirisha zaidi mchezo wa pili ambapo pia kiungo huyo alicheza dakika zote tisini kwa kiwango kizuri sana,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kubainisha kuwa, baada ya mchezo huo wa pili uliochezwa Tunisia wikiendi iliyopita, Fadlu alimpa jukumu kipa wake, Moussa Camara kwenda kuzungumza na Conte ambaye anatoka naye nchi moja ya Guinea.
“Baada ya mchezo wa Tunisia kocha Fadlu alimuelewa zaidi kwani alicheza vizuri na makeke yake yalimkosha.
“Kocha alimtuma kipa Camara akazungumze naye kama njia ya kumshawishi, ni wazi kuwa ameona kitu cha tofauti kipo ndani yake ambacho kinaweza kuongeza kitu kikosini kwetu,” kilibainisha chanzo hicho huku dirisha dogo la usajili Bongo likifungwa wiki ijayo.
Katika mchezo huo wa pili, Simba ilishinda bao 1-0 kupitia Jean Charles Ahoua dakika ya 34, huku ule wa kwanza mfungaji akiwa Kibu Denis aliyefunga yote mawili.
Balla Moussa Conte ni nani?
Ni kiungo wa ukabaji mzaliwa wa Kamsar nchini Guinea ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo cha ushambuliaji.
Kiungo huyo aliyezaliwa Aprili 15, 2004 akiwa na miaka 20 hivi sasa, amekuwa mhimili mzuri ndani ya kikosi cha CS Sfaixien alichojiunga nacho Februari Mosi, 2023, huku malezi yake ya soka akiyapata katika Kituo cha Academie La Louvia kilichopo kwao Guinea.
Katika kikosi cha CS Sfaxien chenye mchanganyiko wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Mali, Algeria, Tunisia, Guinea na Ivory Coast, kiungo huyo ni nyota wa tano kati ya wenye thamani kubwa klabuni hapo.
Katika listi ya wachezaji wa CS Sfaxien wenye thamani kubwa, anaanza Mohamed Nasraoui (bilioni 1.8) sawa na Hichem Baccar na Mohamed Dhaoui ‘Cristo’. Anayefuatia ni Aymen Dahmen (bilioni 1.7) kisha ndiyo Balla Moussa Conte (bilioni 1.4).
Kwanini Fadlu anamuhitaji Conte?
Katika kikosi cha Simba, tayari kuna viungo wakabaji watatu wa kimataifa ambao ni Fabrice Ngoma, Debora Mavambo na Augustine Okejepha. Kati ya wachezaji hao, siku za karibuni Ngoma ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika Juni 30, 2025, ameonekana kuwaka sana kiasi cha kuhatarisha nafasi za wenzake ambao wamejiunga na kikosi hicho mwanzoni mwa msimu huu huku yeye akiandaliwa mkataba mpya.
Mbali na hao, pia kuna wazawa Mzamiru Yassin ambaye yupo kikosini hapo tangu Julai 2016 mkataba wake ukitarajiwa kumalizika Juni 30, 2026 na Yusuph Kagoma aliyetua msimu huu akitokea Fountain Gate.
Conte ambaye kiumri bado mdogo, anatakiwa na Fadlu katika kufanikisha projekti yake ya muda mrefu kuijenga timu hiyo kwani tangu ametua Julai 2024, asilimia kubwa ya wachezaji aliowasajili ni chini ya miaka 25, hivyo kiungo huyo ni mtu sahihi kwake kwa faida ya baadaye.