KATIKA sherehe za mwishoni mwa mwaka, Bernard Kamungo ambaye anaichezea FC Dallas ya Ligi Kuu Marekani ‘MLS’ alikuwa Tanzania kwa ajili ya mapumziko. Mwanaspoti lilipata nafasi ya kuzungumza naye kwa dakika 20 katika moja ya hoteli zenye hadhi ya nyota tano jijini Dar es Salaam kuhusu mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ndoto yake ya kuichezea Taifa Stars na masuala mengine.
Kamungo, ambaye ameonyesha kipaji cha kipekee kiasi cha kuwa gumzo Marekani kutokana na safari yake, anajivunia kushiriki katika michuano ya kimataifa na pia anazingatia umuhimu wa jamii na familia katika mafanikio yake.
Wengi wanamkumbuka Kamungo kwa bao aliloifunga timu ya Lionel Messi ya Inter Miami katika mechi ya kuwania kuingia robo fainali ya Kombe la Ligi na baadaye akapiga picha uwanjani akiwa na mshindi huyo mara saba wa tuzo ya Balon d’Or. Siku hiyo, Messi alifunga bao la kwanza na la nne katika sare ya 4-4 kabla ya Inter Miami kushinda kwa penalti 5-3. Kamungo alifunga bao la pili la FC Dallas.
Kamungo alizaliwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, Tanzania, miaka 23 iliyopita akikulia katika mazingira magumu.
Mazungumzo yetu yalianzia hapo na kusema hapakuwa na vifaa vya kuchezea, lakini alijifunza soka kwa namna ya kipekee, na alijikumbusha hilo kwa kucheza na watoto wa mtaani wakati akiwa Kigoma, mpira wa kufuma na makaratasi.
“Tulikuwa hatuna pesa za kununua mpira,” anasema Kamungo. “Ililazimu kutengeneza mipira yetu wenyewe kwa kutumia mifuko au vitu vingine, kisha mimi na wachezaji wenzangu tulikuwa tukicheza mitaani dhidi ya watu wengine.”
Wakati huo, Kamungo hakuwa na ndoto ya kucheza soka kilipwa.
Mabadiliko makubwa yalikuja alipoingia katika miaka ya ujana. Kwa msaada wa shirika la International Rescue Committee, Kamungo na familia yake walihamia Abilene, Texas, Marekani. “Kilikuwa kipindi cha kushangaza kwangu kwa sababu tulipofika Abilene, familia yangu iliweza kupata chakula. Hicho ndicho nilichokuwa nataka. Nchini Tanzania ilikuwa vigumu kwa wazazi wangu kupata chakula. Wakati mwingine nakumbuka tulikula mara moja kwa siku na hiyo ilikuwa ni kawaida. Lakini tulipofika Abilene, nikaanza kula milo yote ya siku, sasa ningeweza kula mara tatu au nne kwa siku, chochote nilichotaka.”
Safari ya Kamungo katika soka ilianzishwa na kaka yake, Imani Kamungo (ambaye alikuwa pembeni yetu wakati wa mahojiano haya), aliona uwezo mkubwa katika mdogo wake. Bernard alicheza soka katika shule ya Abilene, ambapo alikuwa nyota wa timu hiyo, licha ya kuwa amejifunza mchezo huo mitaani kwenye kambi ya wakimbizi.
Imani aliona kama ndugu yake anaweza kufika mbali zaidi, na alikusudia kumsaidia kufikia ndoto zake. Bernard alikataa kuwa mchezaji wa kulipwa kwa kipindi kirefu, akisema: “Wakati huo, sikuwahi kujiona kama mchezaji wa kulipwa,” anasema.
Licha ya Bernard kuwa na shaka, Imani alimsajili kwa ajili ya majaribio ya wazi na timu ya North Texas SC, timu ya akiba ya FC Dallas. Kamungo aliwakosha waandaaji wa majaribio na huo ndio ukawa mwanzo wa safari yake.
Akimuongelea Bernard, Imani anasema; “Nadhani ni Mungu tu aliweka msukumo ndani yangu, nimekuwa nikijivunia sana uamuzi nilioufanya wa kuchochea kwa ndugu yangu kuonyesha kipaji chake.”
Msimu uliofuata, Kamungo aliongoza timu ya North Texas SC kuwa mfungaji bora na hatimaye alikubaliwa kuichezea FC Dallas. Kutoka soka la shule hadi Ligi Kuu ya soka ya Marekani (MLS) katika kipindi cha chini ya miaka miwili, Kamungo alijiona akifikia kilele cha mafanikio haraka kuliko alivyodhani.
Katika mwaka wa 2023, Kamungo alifunga bao la ushindi katika mechi yake ya nyumbani, na miezi michache baadaye alifunga tena bao la ushindi katika mechi yake ya kwanza kwa timu ya wakubwa. Alionyesha kiwango cha juu kwenye Kombe la Ligi (League Cup), ambapo alifunga mabao matatu na kutoa asisti tatu katika michezo mitatu, akithibitisha uwezo wake wa kuwa mmoja wa wachezaji bora wa pembeni katika mashindano hayo.
Changamoto iliyofuata ilikuwa ni dhidi ya timu yenye nyota wengi katika historia ya MLS, Inter Miami, iliyokuwa na Lionel Messi, Sergio Busquets, na Jordi Alba wachezaji watatu walioshinda kila kitu katika ngazi ya klabu. Katika mechi hiyo ya raundi ya 16 ya Kombe la Ligi, Kamungo alifunga bao baada ya kupita mabeki wawili wa Miami kwa ustadi mkubwa na kumshinda kipa wao.
Hata hivyo katika mchezo huo, FC Dallas ilishindwa baada ya sare ya 4-4 kufuatiwa na mikwaju ya penalti, ambapo Messi na timu yake walishinda. Lakini kwa Kamungo, ilikuwa ni ushindi wa kipekee kwani alifunga mbele ya kaka yake, Imani, kwa mara ya kwanza akiwa uwanjani.
Anasema; “Sijui hata nieleze vipi. Ni moja ya yale mambo ambayo hayajapata kutokea, kwa sababu sikuwahi kufunga mbele ya Imani. Hilo lilikuwa mara yangu ya kwanza kufunga mbele yake, na ilikuwa dhidi ya Messi.”
“Nilimgeukia tu na kumwambia, ‘bao hili ni kwa ajili yako.” Kwa sababu alifanya mengi ili niwepo hapa nilipo. Najiuliza ni furaha gani kuona ameniona nikiweza kufunga.”
Juni 2023, Kamungo alipokea wito wake wa kwanza kujiunga na timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika la 2023 dhidi ya Niger. Hii ilikuwa ni hatua kubwa kwa Kamungo, ambaye alikuwa na hamu ya kuwakilisha nchi yake kwenye uwanja wa kimataifa.
Kwa bahati mbaya winga huyo hakutumika na hakutaka kueleza zaidi kuhusu nini kilimkwamisha lakini Oktoba 8, 2023, alipata wito mwingine, huu ukiwa ni kutoka kwa timu ya taifa ya Marekani ya chini ya umri wa miaka 23 kwa ajili ya michezo ya kirafiki dhidi ya Mexico na Japan.
Kamungo alicheza mchezo wake wa kwanza timu ya taifa ya wakubwa ya Marekani Januari 20, 2024, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Slovenia, akionyesha kwamba safari yake ya kimataifa sasa ilikuwa imeanza rasmi.
“Ni ndoto yangu kucheza kwa timu ya taifa ya Tanzania, lakini pia ni furaha yangu kuwakilisha Marekani kwa sasa. Nimejivunia sana kuona kwamba kila kitu kinanifuata na ninaendelea kupambania ndoto zangu.”
Kwa sasa, Kamungo anaangazia mustakabali wake katika soka la kimataifa, akitaka kuwa mmoja wa wachezaji bora wa dunia.
“Kila hatua niliyofikia ni matokeo ya bidii na kujitolea. Sina uhakika nini kitakuja baadae, lakini mimi ni mchezaji anayependa changamoto. Niko tayari kuchukua kila fursa inayokuja mbele yangu.”