Dereva wa Serikali aliyedakwa akiendesha pikipiki huku amelewa, mwajiri atoa neno

Morogoro. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Zahra Michuzi amesema tayari hatua zimeanza kuchukulia za kinidhamu dhidi ya mtumishi wa halmashari hiyo, Gervas Joshua (39) aliyekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuendesha pikipiki mali ya halmashari hiyo akiwa amelewa kupita kiasi.

Mapema leo asubuhi Jumatano Januari 8, 2025 akizungumza na waandishi wa habari ofisini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema tukio hilo lilitokea Januari 6, 2025, dereva huyo alikutwa akiendesha pikipiki aina ya Honda, mali ya Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akiwa amelewa.

“Huyu dereva wa Serikali baada ya kufanyiwa vipimo, alikutwa na kiwango cha ulevi cha alcohol 99.9, ambacho ni kiwango cha juu. Ni kosa kisheria mtu kuendesha chombo cha moto akiwa amelewa, anaweza kuhatarisha usalama wake na wa watumiaji wengine wa barabara,” amesema Kamanda Mkama.

Amesema uchunguzi utakapokamilika, dereva huyo atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Michuzi amesema mtumishi huyo anafanya kazi katika idara ya michezo na utamaduni na kwamba, pikipiki ya Serikali alikabidhiwa kwa ajili kutumia kwenye shughuli zake za kiutumishi.

“Ni kweli kabisa huyu ni mtumishi wa Halmashauri ya mji wa Ifakara na mimi kama mwajiri nilipokea taarifa hizi kutoka Jeshi la Polisi, hivyo kama mwajiri zipo hatua ambazo nimeanza kuchukua ili kutoa fundisho kwa wengine,” amesema Michuzi.

Wakati huohuo, Kamanda Mkama amesema  jeshi hilo limemkamata dereva wa basi dogo la abiria, Abdul Salumu kwa tuhuma za kubeba abiria wengi kuliko uwezo wa basi hilo.

“Basi hilo lina uwezo wa kubeba abiria 26, lakini dereva huyo alibeba abiria 46, hivyo kuzidisha abiria 20,” amesema Kamanda Mkama.

Aidha, amesema jeshi hilo linamshikilia kondakta wa basi linalomilikiwa na Kampuni ya Simiyu, Athumani Rashidi (54) kwa tuhuma za kuzidisha abiria.

“Huyu kondakta, ambaye ana wajibu wa kusimamia upakiaji sahihi wa abiria, aliruhusu abiria zaidi ya 70 kupanda kwenye basi lenye uwezo wa kubeba abiria 65. Tumemkamata na kushusha abiria wote waliokuwa wamezidi,” amesema Kamanda Mkama.

Kamanda Mkama anewahimiza madereva na makondakta kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kuhatarisha maisha ya abiria.

Related Posts