Fountain Gate hakuna kulala, warejea kambini

LICHA ya Ligi Bara Kuu kusimama kwa miezi miwili, kikosi cha Fountain Gate kimeamua kurudi mapema kambini kikipanga kuanza Jumamosi kujiweka fiti tayari kwa duru la pili la ligi ya msimu huu.

Fountain ambayo ipo nafasi ya sita kwenye msimamo inatarajia kuingia kambini Januari 11, huku mastaa wa timu hiyo wakitarajia kuanza kuripoti kuanzia kesho, Ijumaa.

Wakati wachezaji wakianza kuripoti siku hiyo, uongozi umesema hadi kufikia Jumamosi utakuwa umemaliza mazungumzo na kumtambulisha kocha mpya baada ya kuachana na Mohamed Muya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Fountain, Issa Liponda alisema timu inatarajia kurejea mazoezini Jumamosi na suala la kocha kabla ya timu kuingia kambini atakuwa ametambulishwa.

“Kuna programu maalum wachezaji wamepewa na wanaendelea nayo, lakini kuanzia Ijumaa wanaanza kuripoti tayari kwa ajili ya kuanza kambi Jumamosi kujifua kwa ajili ya kurejea tukiwa bora mzunguko uliobaki,” alisema Liponda na kuongeza:

“Progamu zimetolewa kwa wachezaji wengi ambao wameingia dirisha dogo lengo ni kurudi wakiwa timamu na kuongeza kuvu kwa kuhakikisha timu inafikia malengo ya kumaliza nafasi tano za juu.”

Akizungumzia suala la kocha, alisema wapo kwenye hatua za mwisho za mazungumzo na mmoja wa makocha bora kutoka Kenya jina lake muda wowote litatangazwa kabla ya timu kuingia kambini. Mwanaspoti linajua timu hiyo inazungumza na Robert Matano.

Related Posts