SIKU chache tangu Mwanaspoti liliripoti kuwa Tabora United ilikuwa hatua ya mwisho kumshusha kipa wa timu ya taifa ya Gabon, mabosi wamekubaliano kutemana na kipa Mnigeria Victor Sochima, huku nyota huyo akisema amefurahi kutimiza malengo ya kucheza soka Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sochima alisema alibakisha mkataba wa miezi sita na timu hiyo, japokuwa baada ya duru la kwanza Ligi Kuu kutopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara, amechukua uamuzi wa kuachana kwa amani ya Tabora asake changamoto mpya.
“Moja ya makubaliano yetu ilikuwa ni kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza, ila mambo nimeona yamekuwa tofauti. Baada ya kuona nimekuwa na wakati mgumu kikosini niliamua kukaa na viongozi ili tuvunje mkataba uliobaki baina yetu,” alisema Sochima.
Kipa huyo aliyezaliwa Januari 8, 1999, alijiunga na Tabora United Agosti 17, mwaka jana, kuziba pengo la Mnigeria mwenzake, John Noble aliyekuwa ameondoka kikosini na kujiunga akajiunga na Fountain Gate.
Sochima alitua Tabora United akitokea Rivers United akiwa amezichezea Jigawa na Heartland zote za Nigeria, ambapo ameshindwa kucheza mara kwa mara mbele ya makipa wenzake, Hussein Masalanga na Haroun Mandanda.
Nyota huyo alianza mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara akiwa na timu hiyo kati ya 15 msimu huu ambao Tabora United ilichapwa mabao 4-2, dhidi ya JKT Tanzania, huku akicheza dakika 60 baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu alipoudaka mpira nje ya eneo la 18.
Tayari mabosi wa Tabora United wameanza kutafuta mbadala wake na walikuwa hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kipa wa timu ya taifa ya Gabon, Jean-Noel Amonome aliyeichezea Amazulu ya Afrika Kusini na AS Arta/Solar7 ya Djibouti.