Nashukuru. Nilimaliza mwaka uzuri. Nawatakieni mwaka mpya wenye heri wote wapenzi wangu na mafyatu wote. Niende kwenye ishu. Kuna mchezo hatari unaanza kufyatua mafyatu hadi baadhi yao wanawafyatua mafyatu waliokataa kufyatuka hadi wakafyatuliwa kirahisirahisi.
Kuna kaugonjwa ka kuombaomba na kukopa njuluku toka kwa Wachina, wamanga, na watasha. Wapo wanaoomba baraka wanapokwenda kukopa! Huduma za kijamii, lazima mafyatu waombe. Wakizipata, wanasifia hata wale wanaotimiza wajibu wao. Kabla ya kula, kuna mafyatu wanaomba. Ila wakati wa kuanza kulima hawaombi.
Kamchezo/kagonjwa kengine ni kuamini au kutemea miujiza feki na uchwara. Juzi nilisikia fyatu aliyekuwa amekwama kituo cha ngwarangwara kule Kawee akisema eti alitoka mikoani kwenda kwa mchunaji, sorry, mchungaji, habithi, sorry, nabii Dar aombewe amalize mgogoro wa kiwanja! Hii ni akili au utaahira?
Kutokana na kuzoeleka kwa kamchezo ka kuombaomba na kuamini miujiza feki na uchwara, kuna wajanja wachache wanaotaka kuwa karibu na wanene wa kisiasa ili wawafyatue mafyatu wanaokuja na gia ya kuombea kaya. Mfano, wanaomba mvua wakati wanaharibu mazingira wasijue suluhu ni kutunza mazingira.
Wanaomba amani katikati ya dhuluma, utekaji na vurugu wakati suluhu ni kutenda haki na kupambana na ukapuku wa kutengenezwa na ufisadi. Wanaomba furaha wakati kila kitu ni karaha. Wanaomba utajiri bila kutaka kuchapa kazi na kutetea haki zao. Wanaombea kaya badala ya kuiambia ukweli kuwa iendavyo sivyo! Nawaambieni.
Mtaomba hata uchi, hayo mnayoomba hamtapata. Bwana God siyo njinga mjue. Kawapa uchumi mnaukalia halafu mnaendekeza kubomu na kukopa, na isirafu. Kawapa madini bwerere. Mnashuhudia yakivushwa kila uchao halafu mnakwenda kuomba hukohuko yapelekwako. Mafyatu hawachapi kazi. Wameshikilia ushirikina wa kuomba, halafu wanategemea waletewe maendeleo. Kivipi?
Majizi manene yanafyatua njuluku ndefu. Yakifa tunaomba yaingie peponi. Mengine yanapiga soga makazini badala ya kuchapa kazi. Kuna uzururaji na matumizi mabaya ya rasilimali za kaya yanayofanywa na baadhi ya mafyatu wapaswao kuwafyatua wasifyatuliwe. Halafu eti mnategemea kaya itajirike. Vipi? Acheni kujigeuza ombaomba bila sababu za msingi wala ulazima.
Mnachohitaji si kuombewa bali kuambiwa ukweli. Hamhitaji dua na sala, bali uadilifu na ukweli. Wanaowafyatua wakiwaaminisha wanaweza kuwaombea, wanahitaji kuombewa sana tu. Sasa mie siwaombei. Nawaambia. Mnajichelewesha kwa ushirikina wenu mnaoita imani.
Waliobukua historia wanajua. Walipokuja watasha na vitabu vyao vya kuomba, walituambia tufumbe macho tuombe. Tulipoyafumbua, tulijikuta wametufyatua kwa kutupa vitabu wakafyatua ardhi na mali zetu. Hawa wanaotufundisha kuomba kwa kila kitu, kwao hawaombi. Walituletea ukoloni na utumwa hivi hivi kutokana na ujinga na uzwazwa wetu. Mnadhani akina Mkwawa, Mirambo, Nyungu ya Mawe na Mchonga wangeomba, mngekuwa huru leo?
Hata kama kuomba kunalipa, si kwa wale wanaoombewa bali wanaowaombea. Hamjaona biashara ya neno na miujiza vilivyogeuka dili? Badala ya kujihangaisha na kuchapa kazi, waombaji wanawaibia mazwazwa waliokata tamaa wanaoamini miujiza uchwara. Japo wanaiba kihalali, wizi ni wizi, tatizo ni kuufumbia macho na kuubariki kutokana na ugonjwa wa kuomba na ushirikina.
Jitu linaanza kijikanisa uchwara tena kwenye banda la tope. Punde si punde linaangusha mahekalu. Ukiuliza miujiza gani, unaambiwa neema za God. Mingine inatuhumiwa kuuza bwibwi au kusaidia wafanyabiashara wakwepa kodi kupitisha bidhaa bila kulipa kodi kwa sababu dini zimesamehewa. Huu nao ni udhaifu wa kimfumo.
Mnawasamehe kulipa kodi, kwani, nyinyi ndo mliwalazimisha wafanya biashara ya kuuza neno? Au ni kwa vile mmerithi tabia hii ambapo wakoloni walizawadia dini kodi kwa sababu zilizowasaidia kututawala kirahisi baada ya kutupeleleza na kutoa siri zetu kwa wakoloni?
Kwa mujibu wa Madison Trust Company, Kanisa la Roma linashikilia nafasi ya kwanza kuwa na ardhi kuliko taasisi yoyote duniani. Lina heka zipatazo 177,000,000. Kwa kulinganisha, ukubwa wa ardhi inayomilikiwa na Vatican, ni kubwa kuliko taifa la Ufaransa ambalo lina ukubwa wa eka 166,757,337. Ni zaidi ya nusu ya eneo la Tanzania yenye ukubwa wa eka 234,108,380.
Kuonyesha mnyororo na ukoloni, familia ya kifalme ya Uingereza nayo inaongoza kwa kuwa na ekari 6,600,000,000. Kinachostua, ni kwamba mamilioni yote ya ardhi yanayomilkiwa na wakoloni hawa, licha ya kuingizia mabilioni ya dola, yalinyakuliwa bila kulipa chochote hasa kwa bara la Afrika.
Kwa waliosoma historia na kuielewa wanajua namna wamisionari walifyotufyatua. Walitwambia tutubu dhambi halafu wakajua udhaifu wetu na kuwapa taarifa mataifa ya kikoloni yaliyowatuma ikawa rahisi kututawala. Mbali na hili, ukiangalia namna makanisa hasa ya Kirumi yalivyo na ardhi chekwa, unagundua kuwa hakuna kitu walifanya kama kunyakua ardhi.
Tumalizie. Mliomba, mnaomba, mtaomba ila mjue mnakwepa tatizo kwa kutafuta suluhu ya tatizo lisilokuwapo. Mtaomba hata uchi. Matatizo yenu yatabaki palepale na sanasana yataongezeka.