Dar es Salaam. Ushindani unaoendelea katika nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), unatajwa kuwapa wakati mgumu wagombea wa nafasi ngazi za mabaraza ya chama hicho.
Ugumu huo, unatokana na kile kinachotajwa kuwa, inamlazimu mgombea kujipambanua upande anaouunga mkono kati ya Tundu Lissu na Freeman Mbowe wanaogombea uenyekiti wa chama hicho.
Mbowe anatetea nafasi hiyo aliyoingoza kwa miaka 21 huku Lissu ambaye kwa sasa ni Makamu-Bara anawania kiti hicho. Uchaguzi utafanyika Januari 21, 2025, katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Hali hiyo, inaendelea huku Kamati Kuu ya Chadema, ikiwa kwenye mchakato wa kuwafanyia usaili na kuwateuwa makada 300 waliotia nia ya kugombea nafasi mbalimbali ndani ya mabaraza hayo ya vijana (Bavicha), wanawake (Bawacha) na wazee (Bazecha).
Hata hivyo, wagombea wengine wa nafasi za mabaraza wanasema kuna wakati wapiga kura wanawauliza kati ya Lissu na Mbowe ni nani wanamuunga mkono, huku wengine wakidai ushawishi walionao unajitosheleza na hawana sababu ya kuwa na upande.
Uchaguzi wa Bavicha na Bazecha utakuwa Januari 13 huku wa Bawacha utafanyika Januari 16.
Mchuano huo haupo tu kwenye mabaraza bali hata kwenye ujumbe wa kamati kuu ambayo kingany’anyiro ni kikubwa.
Akizungumzia hilo, Mgombea wa Uenyekiti wa Bazecha, Suzan Lyimo amesema ingawa si changamoto kubwa, lakini wapigakura wamekuwa wakimuuliza kutaka kujua yuko upande gani.
Inapotokea hali kama hiyo, amesema anazungumza na mwanachama husika kumuelimisha juu ya umuhimu wa wagombea wote kwa chama hicho.
“Kuna wakati mtu anakuuliza wewe upo upande gani, namuelimisha kuhusiana na kwamba chama ni cha wote atakayeshinda tutafanya naye kazi, kwenye chama hajaletwa mtu,” amesema.
Kwa upande wa mgombea wa uenyekiti Bawacha, Celestine Simba amesema kuwashawishi wapigakura ni hekima ya mtu binafsi, haihitaji kujiegemeza na upande wowote.
“Ni suala la hekima ya mtu na namna anavyoweza kuwasiliana na wapigakura, kwa sababu kila baraza lina wapigakura wake. Joto la juu linaongeza hamasa kwenye mabaraza ili kila mtu aweze kujisimamia badala ya chama kuingilia mabaraza,” amesema.
Catherine Ruge anayegombea kutetea nafasi yake ya Katibu Mkuu wa Bawacha, ameeleza kwa uzoefu na utendaji wake, hana sababu ya kuonyesha upande, kwani anauzika.
“Nimekuwa kiongozi kwa muda mrefu, nimeonyesha uwezo na nauzika. Lakini hata wapigakura wangu hawalingani na wale wa chama,” amesema.
Amesema ni wapigakura watano pekee ndiyo wanaoshiriki uchaguzi wa mwenyekiti Taifa, hivyo hapati tabu ya kuonyesha upande.
Mmoja wa wagombea wa kamati kuu aliyeomba hifadhi ya jina amesema: “Lissu na Mbowe wanatupa wakati mgumu sana, ukionekana kumuunga mkono mmoja, unakosa kura za mwingine, ukiwa katikati huoneshi upande unaweza kukosa kura kwani wapigakura wanakuwa hawakuelewi elewi.”
“Yaani uchaguzi wa mwaka huu kwa kweli ni shughuli sana. Lakini kila mmoja anapambana kivyake ila ni kazi kwelikweli.”
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, amesema kama Chadema wanaelewa minyukano yao inalenga kupata uongozi utakaowatengenezea njia mpya, hakutakuwa na ugumu kwa wagombea wa nafasi nyingine.
Amesema kama hawaelewi hilo, wagombea wa nafasi nyingine zikiwamo za mabaraza, watakabiliwa na ugumu wa kulazimika kuonyesha mgombea wa uenyekiti wanayemuunga mkono ili wapate kura za wafuasi wake.
Hata hivyo, ameeleza athari za hilo ni kwamba mgombea wa nafasi ya baraza hatajua upande gani sahihi wa kuungana nao ili kupata kura za kutosha.
Dk Masabo amesema kilichomo ndani ya Chadema kwa sasa kinawapa changamoto wengi kuelewa kwa sababu hakikuwahi kutokea tangu siasa za vyama vingi zilipoanza.
Hata hivyo, ameeleza ushindani wa ndani ya vyama uliwahi kuelezwa na Mwalimu Julius Nyerere katika moja ya vitabu vyake, akifafanua dhana ya vyama vya upinzani akihusisha na msingi wa upinzani wenyewe.
Ameeleza kinachoshuhudiwa Chadema sasa ndicho kilichokuwepo kwa Tanu na ANC, vyama ambavyo pamoja na kushindana lakini vilikuwa vinapigania jambo moja, ukombozi wa Taifa.
Kwa sababu wagombea wote ndani ya Chadema wanaongozwa na itikadi moja, amesema upinzani wao si halisi na wanapaswa kurudi pamoja baada ya uchaguzi.
“Sasa suala la kujua kama Chadema nao wanaelewa kuwa upinzani wao si halisi na wanapaswa kurudi pamoja baada ya uchaguzi, sina uhakika nalo,” amesema.