Lindi. Madereva wa mabasi yanayofanya safari kutoka Stendi Kuu ya Lindi kuelekea Masasi mkoani Mtwara na Nachingwea, Liwale na Ruangwa, wamegoma kuendelea na safari kwa madai ya kufungiwa leseni na kuzidishiwa faini kutoka kwa askari wa kitengo cha usalama barabarani mkoani Lindi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Januari 8, 2025, Bakari Saidi ambaye ni dereva wa basi linalofanya safari zake kuelekea Masasi, amedai kuwa biashara imekuwa ngumu kutokana na kupigwa faini zaidi ya mara tatu kwa siku moja, hali inayowafanya washindwe kufikia hesabu za wamiliki.
“Hali imekuwa ngumu sana. Tumekuwa tukigombana na mabosi wetu kutokana na kushindwa kufikisha hesabu zao kwa siku. Hii inatokana na kupigwa faini zaidi ya moja kwa siku na wakati mwingine hata kama huna kosa, unaandikiwa faini,” amedai Saidi.
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Lindi, James Makumu kuhusia na hilo na amesema hakuna dereva aliyeandikiwa makosa zaidi ya matatu kwa siku. Hata hivyo, amesema madereva wengi wanavunja sheria ya barabarani kwa makusudi huku wengi wao wakiendesha mabasi hayo kwa mwendo wa kasi.
“Siwezi kuona damu inamwagika mkoani Lindi kwa sababu ya uzembe wa madereva. Hakuna dereva anayeonewa. Niwatake madereva kufuata sheria, kuendesha kwa mwendo unaotakiwa na kuhakikisha wanapakia abiria kulingana na uwezo wa basi lake,” amesema Makumu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva amewataka madereva kurudi barabarani huku akiahidi kukutana na viongozi wao ili kujadili na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Naomba madereva wote waendelee na kazi yao ya kubeba abiria. Nitakutana na viongozi wenu pamoja na wenzangu ili tujadili na kuondoa changamoto zote,” amesema Mwanziva.
Jamila Abdalla, ambaye ni msafiri aliyekuwa akielekea Masasi, ameomba Serikali kuchukua hatua za haraka kutatua mgogoro huo ili huduma za usafiri ziweze kurejea.
“Naiomba Serikali ikae na madereva ili waondoe tatizo lililopo. Leo tunapata adha kubwa sana,” amesema Abdalla.
Licha ya maelekezo ya Mkuu wa Wilaya, madereva hao wameendelea na mgomo huo.