Mbowe vs Lissu: Wanavyoubeba mustakabali Chadema baada ya uchaguzi

Mjadala mkubwa umeendelea nchini tangu Desemba 12, 2024 baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu kutangaza kugombea uenyekiti wa chama hicho, akishindana na Mwenyekiti, Freeman Mbowe.

Licha ya kwamba tayari wagombea wanne wamechukua na kurejesha fomu kuwania nafasi hiyo, ushindani mkubwa uko kati ya vigogo hao wawili; Mbowe na Lissu na kumekuwa na hatari ya kukipeleka chama hicho shimoni.

Wawili hao pamoja na wafuasi wao wamekuwa wakitupiana maneno, kila upande ukijaribu kuonyesha uzuri wa mgombea wao huku ikionyesha udhaifu wa mwingine, na katika mchakato huo, wakati mwingine lugha zinazotumika siyo za staha.

Upande wa Mbowe wanamwelezea Lissu kama kiongozi mwenye mihemko, asiyejua kipi cha kuzungumza hadharani na kwamba amekuwa akitoa siri za vikao vya kamati kuu, jambo ambalo ni kinyume cha katiba yao.

Kadhalika, upande wa Lissu unaeleza kwamba Mbowe amekaa madarakani kwa muda mrefu wa miaka 20, hivyo amechoka na hawezi tena kuongoza mabadiliko ambayo wanayataka. Pia, wanamtuhumu kushirikiana na CCM kwa mlango wa nyuma kupitia maridhiano.

Minyukano hiyo imeanza kuacha nyufa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani. Maswali ya msingi yamekuwa ni; je, nini mustakabali wa taifa hilo baada ya uchaguzi? Miamba hiyo ya Chadema itaendelea kuwa pamoja baada ya uchaguzi? Nini mustakabali wa chama hicho?

Wadau mbalimbali wa siasa nchini wanajadili mustakabali wa chama hicho baada ya uchaguzi wa Januari 21, mwaka huu, utakaohusisha wajumbe 1,500 kutoka katika mikoa yote nchini katika kufanya uamuzi wa mwisho.

Wanasema minyukano hiyo haiwezi kukiacha chama hicho salama, kwani imevuka hatua ya ushindani wa kisiasa na kuingiza chuki ndani yake, jambo ambalo ni vigumu kulishughulikia kisiasa na watu wakakubaliana mara moja.

Aliyewahi kuwa mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu anasema anakusudia kuwapatanisha Mbowe na Lissu ili waweze kukubaliana, huku akieleza kwamba hali hiyo ikiendelea, chama hakiwezi kubaki salama.

“Niko Moshi, kuna hatua nataka kuzichukua za kuwafanya Mbowe na Lissu waongee na wapangane, aina ya uchaguzi unaoendelea ndani ya chama inaonyesha watu wamekamia, ni lazima, ni lazima…” anasema.

Anasema katika kujaribu kutatua mzozo huo, atatumia njia mbili, ikiwemo ya kuwafikia moja kwa moja na kupitia kwa watu wengine ili kuhakikisha mwafaka unapatikana.

“Ni ngumu chama kubaki salama baada ya kwisha kwa uchaguzi huu, kwa sababu kwa muda mrefu kuna msemo unaosema ‘kwa uchanga wetu tunapangana kuliko kushindana kama hivi’,” anasema Komu.

Komu anasema hatua iliyofikiwa katika chama hicho ni mbaya kwa sababu mwisho wa siku chama kitabaki vipande vipande, huku akisisitiza kwamba kuna uwezekano kwa siku zilizobaki kutuliza hali hiyo.

“Suluhisho ni kukaa na kumaliza tofauti, watu wamekuwa na migogoro mikubwa kama Kenya, wenzetu wanakaa na wanamaliza, iweje ishindikane hapa kwetu, tatizo linalosumbua ni dhana, watu hawajafika hatua ya kusema nipishe wengine,” anasema.

Anasema ili kutibu hali hiyo ni lazima kuweka ukomo wa uongozi kwenye Katiba kwamba ukiwa mwenyekiti kwa muda fulani na ikifikia wakati huhitajiki, basi kaa pembeni.

“Tatizo la viongozi wa vyama vingi vya upinzani hapa nchini wanafikiri vyama ni mali yao, wanashindwa kutambua kama ni mali ya umma na hata wanaovutana Chadema, hawakuanzisha chama, kilianzishwa na watu wengine,” anasema.

Komu anasema bahati isiyokuwa nzuri kinachoendelea Chadema kwa sasa, makundi hayo yameingia kwenye hatua ya kushindana bila kutambua wote bado wanahitajiana.

“Ni kweli kuna kila sababu ya Mbowe kumpisha mtu mwingine, hata kama ingekuwa si Lissu, kwa muda aliokaa kunahitajika mabadiliko akae pembeni kujiangalia na kama unarudi anakuwa na mawazo mengine,” anasema.

Komu anafafanua hoja hiyo akitolea mfano kwa Rais Julius Nyerere wakati anang’atuka madarakani, alikaa baadaye alikuja na kusema anakiona chama kimeoza na kwamba alipokuwa ndani hakujua.

“Alifanya kama operesheni fulani ya kukifanya chama kikae kwenye mstari, sasa ningekuwa mtu wa kushauri ningewataka wapangane, kwani bado kuna vitu Mbowe anaweza kufanya akiwa nje ya Uenyekiti,” anasema.

Komu anasema licha ya joto la uchaguzi kupanda, bado makundi hayo yanaweza kuzungumza na kuyamaliza, kwani hawajachelewa, hata yeye anakusudia kuwa mpatanishi.

Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Azaveli Lwaitama anasema ushindani uliopo unaoendelea kwa chama hicho hauwezi kukifikisha kubaya, isipokuwa wanajaribu kushawishi wajumbe kuwapigia kura.

“Wanaopiga kura ni zaidi ya 1,000 na wanatoka nchi nzima, watu wanajaribu kuwashawishi hawa wajumbe, ndiyo maana unakuta wanachapisha kwenye mitandano ya kijamii na hata katika magazeti,” anasema.

Dk Lwaitama anataja sababu mbili zinazoweza kusababisha chama hicho kuishia kubaya; kwanza, kama mtu hataridhika na matokeo na pili atakayechaguliwa kuwa na kiburi kwa kutaka kuendesha chama bila kuzingatia sheria na miiko.

Anasema katika ushindani huo kuna pande mbili, kuna wanaodai wakishinda watabadilisha mifumo na baadhi wanadai mifumo ibaki kama ilivyo.

“Binafsi nafikiri Lissu anaweza kuwa mwenyekiti bora kuliko mwingine, lakini sasa uchaguzi utaendeshwaje ikitokea mtu analalamikia matokeo, hiyo yenyewe inaweza kuleta mifarakano,” anasema.

Dk Lwaitama anasema inafahamika kila baada ya uchaguzi mahali popote, watu wakiamini uchaguzi mambo yanaenda vizuri, aliyeshinda ameshinda na aliyeshindwa ameshindwa.

“Lakini wakiwa na mashaka juu ya utaratibu wa usimamizi wake inaweza kuleta matatizo, ni muhimu viongozi kuwahimiza wanaosimamia uchaguzi kuendesha kwa haki kama miaka 30 iliyopita,” anasema.

Anasema ni muhimu taratibu zinazotumika siku zote zitumike katika uchaguzi huo na ikitokea mtu analalamika, apate majibu sahihi, huku akitolea mfano kama ilivyokuwa uchaguzi wa Kanda ya Nyasa na Victoria.

“Kulikuwa na malalamiko bila shaka yalitatuliwa na watu inawezekana waliridhika na mifumo ya utoaji haki iliyopo ndani ya chama chao ya kirufaa,” anasema.

Pili, Dk Lwaitama anasema kama atakaye shinda ataheshimu Katiba na kuendesha chama kwa kufuata misingi na matakwa yaliyopo ndani ya chama hicho, haiwezi kutokea shida.

“Akishinda Lissu, tunajua Mbowe atakuwa Mjumbe wa Kamati Kuu yenye kati ya watu 24 hadi 30, tatizo hapa litatokana na iwapo kuna mtu atashinda kwa kutumia ubabe na kutaka kubadilisha Katiba palepale,” anasema.

Dk Lwaitama anasema hata kama kuna mtu atachaguliwa kwa ajenda ya kubadili Katiba, basi itatakiwa azingatie michakato yote badala ya kutaka kubadili mfumo wa uongozi siku hiyo hiyo.

“Msingi wa kubadili Katiba lazima ujengewe hoja na uanzie ngazi za chini na upande, Lissu akishinda sioni tatizo na Mbowe anatabaki kuwa mjumbe,” anasema.

Anasema iwapo Lissu akishinda na kutaka kubadilisha Katiba, Mbowe asiwe mjumbe wa kudumu wa kamati kuu, tatizo linaweza kuanzia hapo, zaidi ya hapo labda utokee msukumo nje ya chama.

Aliyewahi kuwa kada wa Chadema na mbunge wa Bukoba Mjini kupitia chama hicho, Wilfred Lwakatare anasema ushindani ulioibuka kuelekea katika uchaguzi huo, haoni kama unaweza kuwa na athari hasi kwa chama.

“Ushindani ni kawaida, lakini kitu kikubwa kinakuja kama chama, mmejipangaje kukabiliana na hali hiyo? Kama wamejipanga katika hilo, wanaweza kuvuka salama,” anasema Lwakatare.

Mwanasiasa huyo aliyetimkia Chama cha Wananchi (Cuf), anasema ili wavuke salama, wanatakiwa kuzingatia taratibu na kanuni zao na vyombo vinavyosimamia mchakato mzima bila kuegemea upande wowote.

“Wajitahidi kuwa wawazi na kushughulikia mambo kwa wakati, nadhani wakifanya hivyo wanaweza kuvuka salama,” anasema.

Katiba, kanuni zizingatiwe

Mhadhiri wa sayansi ya siasa, Dk Razaro Swai anasema kama watakengeuka misingi ya katiba na taratibu nyingine, lazima chama kitameguka baada ya uchaguzi huo.

“Wakizingatia misingi ya kidemokrasia kwa kuheshimu vipengele vilivyopo, wanaweza kuvuka salama, lazima iwe haki kwa aliyepo madarakani na asiye madarakani kugombea,” anasema.

Dk Swai anasema wasipozingatia hilo huo utakuwa mwanzo wa mpasuko, kufarakana na kudhoofika kwa sababu kilichowafikisha hapo walipo ni mshikamano uliojengeka ndani ya chama.

“Ili chama kiendelee kujijenga kisiasa ni lazima kitawaliwe na mshikamano kwa wanachama wote kwa kuwa wote wanahitajiana,” anasema.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema Chadema kinaweza kubaki salama kwa kuwa yote yanayoendelea ni demokrasia, isipokuwa inategemeana na namna uchaguzi utakavyofanyika.

“Ninachokiona baada ya kuingia Heche, imeleta nguvu mpya kwenye chama kwa kuleta usawa kwa sababu kabla ya hapo, alikuwa Wenje kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti,” anasema mwanazuoni huyo.

Dk Paul anasema uhai umeongezeka, hasa upande wa Lissu na upande wa Mbowe unatakiwa kujipanga zaidi kukabiliana na hoja zinazotoka kila upande.

“Isipokuwa kama kuna upande hautakubali matokeo, inaweza kuleta changamoto nyingine na litakuwa pigo kwa sababu Chadema bado ni oksijeni kwa Serikali na hata kwa chama tawala,” anasema.

Related Posts