Handeni. Maduka mawili ya bidhaa za vyombo na mikate yameteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Jumatano Januari 8, 2025, wilayani Handeni, mkoani Tanga, huku wafanyabiashara wakilalamikia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kushindwa kutoa msaada wa haraka.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Digital leo, wafanyabiashara wa maeneo ya Chanika wilayani Handeni walisema moto huo ulitokea majira ya Saa 8 usiku huku chanzo kikiwa hakijulikani.
Wafanyabiashara hao wamesema licha ya taarifa za moto kutolewa mapema, hakuna msaada uliopatikana kutoka kwa Jeshi la Zimamoto na badala yake moto ulizimwa kwa kutumia maji kutoka msikiti wa jirani.
Mfanyabiashara Pastory Shayo amesema wananchi walijitokeza kwa wingi kusaidia kuuzima hatua iliyosaidia kuzuia usisambaye zaidi kwenye maduka mengine.
Amesema; “Moto ulikuwa mkubwa kiasi cha kushindikana kuokoa mali zilizokuwa ndani ya maduka hayo, zimeungua zote hakuna kilichotoka.”
Mfanyabiashara mwingine, Rajabu Bakari amesema serikali inapaswa kuona umuhimu wa kuipatia wilaya ya Handeni gari jipya la zimamoto.
Amesema licha ya wananchi kuchangia kodi zote muhimu, changamoto ya ukosefu wa gari la kuzimamoto imekuwa ya muda mrefu bila ufumbuzi.
“Zimamoto Handeni walipata taarifa mapema na walifika, lakini hawakuweza kusaidia lolote. Tumetumia maji kutoka msikitini kuzuia moto kusambaa zaidi. Serikali inapaswa kulifanyia kazi suala hili haraka,” amesema Rajabu.
Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Handeni, Ramadhani Matipwili amekiri kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa gari la kuzimamoto.
Amesema taarifa zimeshatolewa kwa mamlaka husika na kuna ahadi ya kutatua changamoto hiyo ili kuimarisha shughuli za uokoaji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Mussa Mkombati amesisitiza umuhimu wa kushughulikia suala hilo mara moja.
Amesema matukio ya moto yamekuwa ya mara kwa mara na kukosekana kwa msaada wa haraka kumeendelea kusababisha hasara kubwa kwa wananchi.
Aidha, Machi 8, 2024, maduka matatu yaliteketea kwa moto katika eneo la Kivesa, ambapo moja pekee lilifanikiwa kuokolewa kwa sehemu ndogo kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuzimia moto.
Hali hii inaonesha haja ya dharura ya kuboresha miundombinu ya uokoaji wilayani Handeni.