Ofisa bima kortini akidaiwa kujipatia Sh38 mil ili awapangishe NHC

Dar es Salaam. Ofisa wa Bima, Said Salum Nyampanguta (29) amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kujibu kesi mbili tofauti za kujipatia jumla ya Sh38 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa watu wawili tofauti kwa madai atawapangisha katika Nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wakati akijua hana mamlaka ya kufanya hivyo.

Nyampanguta amefikishwa mahakamani hapo leo Jumatano, Januari 8, 2025 na kusomewa mashtaka yake na karani wa mahakama hiyo, Shabani Hamad, mbele ya Hakimu Mkazi, Scholastic Odoyo.

Katika kesi ya kwanza, mshtakiwa anadaiwa Mei 11, 2024, saa 11:00 jioni, Mtaa wa Azikiwe, Kata ya Kisutu katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe, alijiapatia fedha taslimu Sh23 milioni kupitia akaunti yake ya CRBD namba 0152330121600 kutoka kwa Hamis Sebulungo kwa lengo la kumpangisha nyumba yenye Plot namba 714/ 11 ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) iliyopo Mtaa wa Jamhuri na Mkwepu.

Inadaiwa mshtakiwa baada ya kujipatia fedha hizo, hakufanya kile walichokubaliana na Hamisi na badala yake, alitokomea na fedha hizo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo alikana shtaka linalomkabili.

Katika kesi ya pili, mshtakiwa anadaiwa Mei 6, 2024, saa 12: 00 jioni katika Mtaa wa Makunganya, Kata ya Kisutu Wilaya ya Ilala, mshtakiwa alijipatia Sh15 milioni kutoka kwa Ulysious Athanas kwa lengo la kupangisha nyumba yenye Plot namba 714/11 ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) iliyopo Mtaa wa Jamhuri na Mkwepu.

Inadaiwa mshtakiwa baada ya kupokea fedha hizo hakufanya kile alichokubaliana na mlalamikaji na badala yake alitokomea na fedha hizo kusikojulikana hadi alipokamatwa.

Mshtakiwa amekana pia shtaka linalomkabili na kuomba apatiwe dhamana.

Hakimu Odoyo ametoa masharti ya dhamana ambayo, alimtaka mshtakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho watakaosaini bondi ya Sh30 milioni kila mmoja kwa kesi zote mbili.

Pia, wadhamini hao wanatakiwa kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh30 milioni au fedha taslimu kiasi cha Sh30 milioni.

Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na amerudishwa rumande hadi Januari 13, 2025.

Related Posts