Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iwaeleze wananchi sababu kutotoa zabuni

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hivi karibuni ilizindua miradi mingi mikubwa, yakiwemo majengo ya kisasa ya soko na kuegeshea magari yenye thamani ya mabilioni ya shilingi.

Miradi hii, iliyozinduliwa wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi imebadilisha sura ya mji wa Zanzibar na ni hatua kubwa ya maendeleo ambayo serikali inayoongozwa na Rais Hussein Mwinyi inafaa kupongezwa.

Ni majengo yanayopendeza na itakuwa vizuri kukiwa hakuna upendeleo katika utoaji wa nafasi za biashara, kodi zikawa zenye unafuu na kubwa zaidi ni kuhakikisha yanatunzwa ili isitokee wakati tunaadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi majengo haya yakawa kama magofu.

Hili ni muhimu sana kwa sababu uzoefu unaonyesha tumekuwa hodari wa kuwa na majengo mazuri, lakini tupo nyuma sana katika kuyatunza.

Hii pia inaonekana katika miundombinu iliyosababisha usafiri kati ya Unguja na Pemba kuwa mzuri, lakini baadhi ya barabara zinaonekana kama ujenzi wake ni wa viwango vya chini kwa vile kazi inayofanyika sasa ni kuweka viraka.

Hata hivyo, yapo baadhi ya mambo hayana budi kuwekwa wazi na hii itasaidia sana kuondoa mashaka juu ya ujenzi wa miradi hii na kuondoa uvumi unaozagaa ambao hauisaidii serikali wala wananchi.

Nayo ni kuwepo uwazi na nafasi ya kuhoji juu ya ujenzi wa miradi hii mikubwa iliyotekelezwa tangu Dk Mwinyi aliposhika hatamu za uongozi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa mfano, yapo malalamiko kwamba utekelezaji wa miradi hii haukuidhinishwa na Baraza la Wawaklishi (BLW) kama sheria ya matumizi ya fedha za serikali zinavyoelekeza.

Tumeambiwa kwamba kazi yote hii imefanyika kwa nia njema na usafi, lakini kitendo cha miradi hii kutopata baraka za BLW siyo sahihi. Kama hili limefanyika basi sio sahihi na ni vizuri mwenendo huu kakomeshwa na wawakilishi wa wananchi ndio wawe wenye uamuzi wa mwisho wa namna ya kutumia misaaada na fedha za walipakodi ambazo Zanzibar inaipata.

Kinacholalamikiwa na hili linahitaji ufafanuzi wa nyaraka na sio maneno matupu ni umma kujua namna mikataba ya miradi hii ilivyofanyika.

Miongoni mwa mambo yanayohitaji ufafanuzi ni kujua kama zilikuwepo zabuni za miradi hii, lini zilitolewa, makampuni mangapi yalishiriki kutaka kuzifanya kazi hizo na kamati gani ya zabuni ndio ilifanya uamuzi na kwa kutumia vigezo gani.

Mengi yanasemwa na wanaosema ni haki yao kufanya hivyo, kama wana mashaka ya kuwepo mizengwe katika utekelezaji wa miradi hii. Mashaka kama haya pia yanasikika juu ya upatikanaji wa mikataba kama ya kuzipa kampuni binafsi kazi ya kukusanya kodi za maegesho ya magari Mji

 Mkongwe na maeneo mengine ya mji wa Zanzibar.

Umma unayo haki ya kujua ada zilizotolewa kwa kuzipa kampuni binafsi kazi hii na kiasi gani cha mapato kinaingia Mamlaka ya Mji Mkongwe au Baraza la Mji wa Zanzibar.

Uwazi ndio njia pekee ya kuondoa mashaka yaliyopo na siyo haki kuwaambia wanaouliza kwamba mambo haya hayawahusu. Kila Mzanzibari ana haki ya kuuliza na hakuna anayestahili kusema ana uwezo wa kuamua atakavyo.

Kama ingekuwa kinachokodishwa ni mali ya mtu binafsi au familia kama ilivyo kwa nyumba au shamba, ingekuwa sawa. Lakini chochote kile kinachomilikiwa na Serikali au taasisi ya umma ni mali ya umma.

Malalamiko yaliyopo ni kwamba hapakuonekana kutolewa zabuni ili waliokuwa wanataka kuchukua jukumu hilo waingie katika zabuni na kushindana.

Kama zabuni zilitolewa ni vema taasisi zinazohusika zikaweka wazi hizo zabuni ili kuwanyamazisha hao wanaodai kwamba katika suala hili kulikuwa na upendeleo, rushwa na ufisadi.

Hapa Serikali ina wajibu wa kujibu hizi hoja na siyo maelezo ya kwamba kulikuwa na nia njema na taratibu zilifuatwa au hao wanaokosoa kubandikwa majina ya kuwa wana yao, hawana uzalendo au sio wenzetu.

Siku zilizopita tuliwahi kusikia baadhi ya viongozi wakitaka Serikali isihojiwe inapofanya jambo zuri na kwamba fedha zinazotumika ni za Serikali ya CCM. Hii siyo sahihi, kwani fedha hizo ni za walipakodi na hata mikopo inayopatikana italipwa na wananchi wa Zanzibar bila kujali ni wa chama gani na siyo wanaCCM peke yao watakaolipa.

Umma unasubiri maelezo na hii itasaidia wananchi kuamini kwamba fedha zao za kodi na hizo za mikopo na misaada zilizobadili taswira ya Zanzibar zilitumika vema na siyo kugeuzwa shamba la mjomba au bibi.

Related Posts