WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma kampuni ya Lake Gas Ltd ambaye atahudumia Mkoa wa Dodoma kwa kuuza kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo 6 pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji ambapo kwa mkoa huo, mradi utagharimu kiasi cha shilingi 406,712,250.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 8 Januari 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa ugawaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku iliyofanyika wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Mhe. Senyamule amefafanua kuwa, katika mkoa huo mitungi ya gesi itauzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 ambayo ni sawa na shilingi 20,825 kwa mtungi mmoja (kutoka bei ya shilingi 41,650).
Amesema Serikali kupitia REA inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wananchi wanaweza kumudu gharama za matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao, kutunza mazingira na kuboresha maisha yao.
“Kupitia mradi huu, wananchi watafaidika na punguzo la bei ya gesi ya mitungi kwa asilimia 50 na watapata mafunzo ya jinsi ya kutumia nishati hiyo kwa usalama na unafuu,” Ameongeza Mhe. Senyamule.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu REA, Mha. Emanuel Yesaya amesema mradi huo umelenga kusambaza mitungi ya gesi 19,530 ya kilo 6 pamoja na vifaa vyake katika wilaya sita (6) za mkoa huo ambapo kila wilaya itapata jumla ya mitungi 3,255.
“Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini na pembezoni mwa miji,” amesema Mha. Yesaya.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Janeth Mayanja amesema mradi huo utapunguza ukataji wa miti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi, vifo vinavyosababishwa na kuvuta hewa chafu inayotokana na kuni na mkaa pamoja na kupunguza ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya familia.
Ameongeza kuwa, mradi huo utapunguza umaskini kwa kuwapa muda zaidi wanawake kushiriki katika shughuli za kiuchumi pindi wanapotumia mitungi ya gesi kama njia mbadala ya kupikia badala ya kuni na mkaa.