Njombe. Katika simulizi ya kesi ya Jamhuri dhidi ya George Sanga na wenzake wawili iliyovuta hisia za wengi wakiwamo viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tulikuletea utetezi wa mshitakiwa wa kwanza katika kesi hii.
Sanga na wenzake walishitakiwa kwa tuhuma za kumuua, Emmanuel Mlelwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kwa vyuo vikuu Mkoa wa Njombe, mauaji yaliyotokea Septemba 19, 2020 wilayani Njombe.
Kiini cha mauaji, kilidaiwa ni hatua ya washitakiwa kuchukizwa na mipango michafu ya marehemu kushawishi wagombea udiwani kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wajiengue ili wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.
Katika sehemu hii ya mwisho, tunakuletea utetezi wa washitakiwa Goodluck Mfuse na Optatus Nkwera pamoja na uchambuzi wa ushahidi uliofanywa na Jaji Dunstan Ndunguru na kuhitimisha kuwa hawakuwa na hatia na kuwaachia huru.
Shahidi wa tatu wa upande wa utetezi, Emmanuel Masonga alieleza kuwa siku ya tukio Septemba 19, 2020, yeye alikuwa Mjini Njombe na mshitakiwa wa kwanza, Sanga wakiendelea na masuala ya kampeni za uchaguzi mkuu.
Alieleza kuwa Septemba 26, 2020 saa 2:00 usiku, yeye, Sanga na Rose Mayemba, walikwenda Kituo cha Polisi Njombe kuuliza kwa nini Thadey Mwanyika anashikiliwa na polisi lakini walipofika hapo wakawekwa chini ya ulinzi.
Masonga alisema aliachiwa na siku iliyofuata alirudi tena kituo cha polisi kuulizia hatima ya Mwanyika na Sanga lakini akaambiwa hawapo kituoni hapo na ndipo Septemba 30, 2020 akaambiwa wamepelekwa mahakamani.
Alikimbilia Mahakama ya Wilaya ya Njombe na kukutana na Sanga akipelekwa gerezani wakati huo akiwa tayari amesomewa mashitaka ya mauaji na kutakiwa kutojibu chochote kwa vile Mahakama haina uwezo kusikiliza shauri hilo.
Utetezi mshitakiwa wa pili na wa tatu
Kwa upande wake, mshitakiwa wa pili, Goodluck Oygen au Mfuse, alijitetea kuwa Septemba 28,2020 saa 11:00 jioni, nyumba yake ilifanyiwa upekuzi na polisi na vitu mbalimbali vilipatikana kikiwamo kitambaa (handkerchief)chenye rangi nyekundu.
Hata hivyo, alisema kitambaa kilichotolewa mahakamani kama kielelezo ni tofauti na kilichochukuliwa na polisi kwa kuwa, hakikuwa chekundu bali kina rangi mchanganyiko na pia kilichochukuliwa hakikuwa na matone ya damu.
Mshitakiwa wa tatu, Optatus Nkwera alijitetea kuwa hakushiriki kwa namna yoyote kumuua marehemu na wala alikuwa hamfahamu wala hakuwahi kumtaja mshitakiwa wa kwanza wala afande Mrisho hakuwahi kuandika maelezo yake.
Baada ya kukamilika kwa ushahidi wa pande mbili, Jaji alisema ni wajibu wa Mahakama kujibu kama Mlelwa kweli ni marehemu na kifo chake hakikuwa cha asili, kama washitakiwa ndio waliomuua kwa dhamira ovu.
Kifo hakikuwa cha kawaida
Akijibu hoja ya kama kifo cha marehemu kilikuwa ni cha asili (natural death) au la, Jaji Ndunguru alisema kwa ushahidi uliopo katika kesi hiyo, hakuna ubishi kuwa Emmanuel Mlelwa ambaye ndio kiini cha kesi hiyo kwa sasa ni marehemu.
Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa kwanza wa Jamhuri uko wazi kuwa Septemba 21,2020 alikuta mwili wa mwanadamu katika dimbwi la maji na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Njombe waliofika eneo la tukio na kuuchukua mwili huo.
“Ingawa wakati huo walikuwa hawajajua mwili huo ni wa nani lakini baadaye ulitambuliwa na baba yake mzazi kuwa ni wa Emmanuel Mlelwa. Ushahidi huu uliungwa mkono na daktari na ndugu kuwa ulikuwa wa Mlelwa.
“Kama kifo kilikuwa cha kawaida ama la, ushahidi unaonyesha mwili wake ulikutwa kwenye maji chini ya daraja, hivyo kwa vyovyote vile haiwezekani kusema kilikuwa ni kifo cha kawaida,”aliendelea kueleza Jaji Ndunguru.
“Ushahidi huo unatoa picha kuwa ama marehemu alianguka mwenyewe kwenye maji au kulikuwa na mkono wa mtu. Lakini daktari aliyeufanyia uchunguzi anasema kiini cha kifo ni kuvunjika kwa uti wa mgongo na kushindwa kupumua.
“Kwa ushahidi huo wa daktari, marehemu ni wazi kabisa kwamba alikabiliwa na kifo cha ghafla na cha kikatili,”alieleza Jaji Ndunguru na kusema hiyo inatosha kujibu hoja kuwa kifo chake hakikuwa cha asili au kawaida.
Akijibu hoja ya kama washitakiwa ndio waliofanya mauaji hayo ama la, Jaji Ndunguru alisema ushahidi wa Jamhuri uliopo katika jalada, unaonyesha hakuna shahidi hata mmoja aliyeshuhudia washitakiwa wakimuua marehemu.
“Ni kwa msingi huo, ushahidi wote uliopo mbele yangu wote ni wa mazingira. Kwa hiyo upande wa mashitaka ulikuwa na wajibu wa kuthibitisha shitaka hilo dhidi ya washitakiwa kwa kuegemea ushahidi wa kimazingira,”alisema Jaji.
“Swali ni kama ushahidi wa kimazingira kama uliopo katika kesi hii unakubalika na unaweza kutumika kuwatia hatiani washitakiwa kwa kuegemea ushahidi wa aina hiyo ama la,”alieleza Jaji Ndunguru.
“Katika kesi hii, hakuna shahidi hata mmoja aliyeshuhudia mauaji isipokuwa ushahidi ni wa mazingira unakubalika kisheria lakini ni lazima upimwe kwa sheria inayosimamia ushahidi wa mazingira ili kumtia mtu hatiani.
“Huo ushahidi ni lazima uwe unawanyooshea kidole washitakiwa na si mtu mwingine yeyote kuwa ndio waliofanya mauaji hayo,”alieleza Jaji na kunukuu sheria na misimamo (case law) iliyojengwa kutokana na kesi mbalimbali.
Jaji alisema kulingana na shahidi wa nne wa Jamhuri, Septemba 26, 2020 mshitakiwa wa kwanza alihojiwa na RCO na yeye akiwepo na kwamba mshitakiwa alikiri kwa mdomo kuhusika na kuwataja washirika ni Ashery Machela na Nkwera.
“Ungamo la mdomo kama yalivyo maungamo mengine ni lazima yapitie kwenye mtihani wa kama lilitolewa kwa hiyari. Uhiyari wa kutoa ungamo unaweza kupimwa kwa kuangalia uaminifu wa shahidi anayeutoa,”alisema Jaji.
“Katika kesi tuliyonayo, shahidi wa nne anasema ni RCO ndiye alimhoji mshitakiwa wa kwanza mbele ya mtu anaitwa Thadey Mwanyika na kwamba ni huyo Thadey ndiye aliyemtaja mshitakiwa wa kwanza na aliitwa ili afunguke kila kitu.
“Kwamba baada ya mshitakiwa kumuona Thadey, hapo hapo akakiri kuhusika na kuwataja wenzake. Wakati shahidi anasema Sanga alihojiwa na RCO, mshitakiwa alisema hakuwahi kuhojiwa na mtu yeyote na alikutana na Thadey kituoni.
“Sasa katika kesi hii, huyo RCO aliyemhoji mshitakiwa mbele ya Thadey Mwanyika na kudaiwa kukiri kufanya mauaji na kuwataja na washirika wenzake hakuna hata mmoja aliyeitwa mahakamani kutoa ushahidi na hakuna maelezo ni kwa nini.
“Katika mazingira haya, ninaona kuwa upande wa mashitaka ulipaswa kuwaita mashahidi hao muhimu ili kupima ushahidi wao. Kwa heshima kabisa, kutowaita kumetoa mashaka ambayo yanampa faida mshitakiwa,”alieleza Jaji.
“Ushahidi mwingine ni wa DNA ambao ni wa shahidi wa tano ambaye ni mkemia wa Serikali. Ushahidi wake uliegemea katika sampuli zilizochukuliwa na watu wengine na kupelekwa kwake, lakini uchukuaji wake haukuzingatia sheria.
“Kwa jumla, hakuna uthibitisho wa nyaraka wa uchukuaji, ufungaji, uhifadhi na usafirishaji ulivyofanyika wa hizo sampuli kama sheria inavyotaka,”alisema Jaji na kugusia utetezi wa mshitakiwa kuwa fulana zilikuwa mpya kwenye nailoni.
Ushahidi kitambaa chenye damu
Jaji alisema ushahidi unaomhusisha mshitakiwa wa pili, Goodluck Mfuse na tuhuma hizo ni kitambaa chekundu cha kujifutia kilichodaiwa kuwa na matone ya damu kilichopatikana nyumbani kwa mshitakiwa alipofanyiwa upekuzi.
“Kulingana na shahidi wa tano, sampuli ya damu iliyochukuliwa kwa ajili ya DNA kutoka katika kitambaa hicho ilioana na sampuli ya damu kutoka mwili wa marehemu,”alisema Jaji akieleza kitambaa hicho kilielezwa ni rangi nyekundu.
“Hati ya upekuzi hakuna mahali popote ilisema kitambaa hicho kilikuwa na matone ya damu na hata shahidi wa tisa hakusema kilikuwa na matone ya damu bali ni kitambaa chenye rangi nyekundu,”alieleza Jaji.
“Nimepata muda wa kukiangalia kitambaa hicho kwa macho yangu na kuona kina rangi mchanganyiko huku rangi nyekundu ikiwa imechukua nafasi kubwa lakini kilikuwa na rangi nyingine ya maua meupe. Hii imeathiri mzizi wa kesi.
“Ninachoona ni kuwa maelezo kuwa kitambaa chekundu kilikuwa na matone ya damu ni maelezo ya baadaye (afterthought) yaliyotokana na mashahidi kufundishwa,”alisema Jaji na kumuona mshitakiwa hana hatia.
Bila kuchambua ushahidi kumhusu mshitakiwa wa tatu, Jaji alisema amepima ushahidi wote kwa umakini mkubwa na kubaini upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa na kuwaachia huru.
Mwisho wa simulizi ya hukumu ya washitakiwa