TARURA RUVUMA YAKEMEA UTUPAJI TAKA KWENYE MIFEREJI NA UCHIMBAJI MCHANGA KWENYE MADARAJA

Wakala wa barabara za Mijini na vijijini Mkoa wa Ruvuma imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu uharibifu wa miundombinu ya barabara, huku ikikemea vitendo vya utupaji taka kwenye mifereji na uchimbaji mchanga kwenye madaraja, kwani vitendo hivi vinarudisha nyuma juhudi za maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Silvester Chinengo, amesema kuwa ni muhimu kwa wananchi kutambua kuwa miundombinu ya barabara ni mali ya wote, na ni jukumu lao kulinda miundombinu hii ili iweze kutumika kwa ufanisi kwani vitendo vya uharibifu kama vile kutupa taka kwenye mifereji au kuchimba mchanga kwenye madaraja, vinazorotesha hali ya usafiri.

Amesema TARURA inashirikiana na viongozi wa vijiji na mitaa ili kuzuia vitendo vya uharibifu na kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara inatunzwa ipasavyo Vilevile wito umetolewa kwa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watashuhudia vitendo vya uharibifu, ili hatua za kisheria zichukuliwe haraka dhidi ya wahusika.

Kwa sasa, mtandao wa barabara katika Mkoa wa Ruvuma unafikia jumla ya kilomita 7,146, ambapo asilimia 65 ya barabara hizo zinapitika vizuri Hata hivyo, TARURA inaendelea na matengenezo ya barabara mbalimbali ili kuboresha huduma za usafiri na kuhakikisha usalama wa abiria.

Mhandis Chinengo amewahimiza wananchi kuwa walinzi wa miundombinu yao, ili kuhakikisha kuwa barabara zinabaki salama na zinatumika kwa manufaa ya wote kwani Miundombinu bora ni nguzo muhimu ya maendeleo, hivyo ni muhimu kuepuka vitendo vya uharibifu na kuchangia katika kulinda rasilimali hizi.

TARURA mkoa wa Ruvuma wanaendelea na usimamizi wa barabara ambapo katika bajeti ya mwaka 2024_2025 wametengewa bajeti ya bilioni 38.394 wanatarajia kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 1445 madaraja 50 Makalavati 57, huku jumla ya mikataba 51 waliyoingia utekelezaji wake ukiwa zaidi ya asilimia 40 ikiwa bado wanaendelea na ujenzi wa barabara viporo utekelezaji umefikia asilimia 70 kwa mradi wa uondoaji vikwazo vya usafirishaji.

Related Posts