Trump aibua mapya sakata la Marekani kuitwaa Canada

Washington. Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump ni kama hajakata tamaa kuhusiana na lake kuifanya Canada kuwa sehemu ya Marekani baada ya kuchapisha picha ikionyesha ramani ya Canada ikionekana kuwa sehemu ya Marekani.

Wakati Trump akichapisha ramani hiyo, mamlaka nchini Canada zimemjia juu na kumjibu kuwa lengo hilo halitotimia katika ulimwengu wa sasa.

Trump amechapisha picha hiyo kwenye mtandao wake wa Truth Jumanne Januari 7, 2024, huku akisisitiza kuwa anaamini baada ya uamuzi wa Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau kutangaza kujiuzulu unaongeza uwezekano wa taifa hilo kuwa jimbo la 51 la kiutawala la Marekani.

Trudeau alitangaza uamuzi wa kung’atuka madarakani juzi kwa alichovieleza vyombo vya habari kuwa ni kuibua kwa migogoro katika Serikali na ndani ya chama chake cha Kiloberali (Liberal Party) jambo linalohatarisha uhai wa taifa hilo.

Kufuatia uamuzi huo, Trump alichapisha ramani inayoonyesha Marekani na Canada ikiwa ni taifa moja bila uwepo mipaka inayotenganisha mataifa hayo.

Baadae, Trump aliendelea kwa kuchapisha picha ikionyesha ramani ya mataifa hayo yakiwa yameingana huku ikiwa imepakwa rangi ya bendera ya Marekani huku akiiambatanisha na maneno “Oh Canada.”

Tovuti ya Russia Today imeripoti kuwa, Trump alipofanya mkutano na waandishi wa habari nchini humo alisema Marekani inaweza kutumia nguvu yake kiuchumi kuwameza majirani zao wa Kaskazini (Canada) huku akitishia kuongeza kodi madhubuti kwenye bidhaa zao

“Futeni hiyo mistari inayoonyesha mipaka ya Taifa lenu na Marekani halafu mtaona namna ilivyo nzuri endapo mtaungana na sisi kwenye masuala mengi hususan ya kiusalama,” Trump alisema.

Muda mfupi baada ya kauli hiyo ya Trump, Waziri Mkuu wa Canada aliyetangaza kujiuzulu, Justin Trudeau, alichapisha kwenye ukurasa wake wa X kuwa “Hakuna hata chembe ya nafasi duniani na kuzimu kuwa Canada itakuja kuwa sehemu ya Marekani.”

Kauli ya Trudeau iliungwa mkono, na Pierre Poilievre, ambaye ni kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Canada (Conservative Party), akionya kuwa: “Haiwezekani Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani.”

Pamoja na kutolea nje pendekezo hilo la Trump, wanasiasa nchini Canada wanasisitiza juu ya kuendeleza mahusiano kati ya mataifa hayo wakati huu ambao taifa hilo linaelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 2025.

Uamuzi wa Trudeau kujiuzulu wadhfa huo pia, alieleza kuwa umechangiwa na kupungukiwa mvuto ndani ya chama chake jambo linalohatarisha kuwa huenda akasababisha kushindwa kwa Chama hicho katika uchaguzi ujao.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts