Vita ya Mbowe, Lissu ina darasa pana kuliko siasa

Nimemwona Wakili Alute Mghwai, kaka wa Tundu Lissu, akisema anamtambua Freeman Mbowe kama mwanafamilia wao. Alute amezungumza kwa hisia kuhusu uhusika wa Mbowe katika uokoaji wa maisha ya Lissu, mdogo wake.

Kila kitu chanzo chake ni Septemba 7, 2017. Watu wabaya kupita kiasi, walimshambulia Lissu kwa risasi zinazokadiriwa kufika 38. Walikusudia zile risasi zichukue uhai wa Lissu.

Haikuwa hivyo. Mungu hakuruhusu wauaji wafanikiwe, japo waliweza kupenyeza risasi 16 kwenye mwili wa Lissu. Mungu ndiye anayeponya, lakini binadamu lazima watengeneze sababu ya uponywaji. Mbowe alicheza mpira mgumu, aliikabili kila hatari iliyokuwa mbele ya Lissu. Mbowe alifanikiwa kumtoa Lissu Hospitali ya Mkoa, Dodoma, akamfikisha Hospitali ya Aga Khan, Nairobi, Kenya.

Alute anasema Mbowe alishiriki kumuuguza Lissu kwa miezi minne. Kitendo hicho ndicho kinawafanya wao kama familia wamwone Mbowe ni ndugu yao. Kuanzia Septemba 8, 2017 mpaka Januari 6, 2018, Lissu alitibiwa Nairobi, Kenya, Hospitali ya Aga Khan, kisha alisafirishwa kwenda Ubelgiji kwa matibabu zaidi.

Kauli ya Alute kuwa Mbowe alimuuguza Lissu kwa miezi minne, inamaanisha ile ya siku ya kwanza ya tukio, Septemba 7, 2017, Dodoma, hadi Januari 6, 2018, alipoondolewa Aga Khan kwenda Ubelgiji. Hiyo ni miezi minne iliyotimia. Ni kipindi ambacho Mbowe macho yake na umakini wake wote, ulielekea wodini alikolala Lissu.

Mapambano ya Mbowe dhidi ya viongozi wa Serikali, waliotaka Lissu akatibiwe Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam. Mbowe aling’ang’aniza Lissu akatibiwe Aga Khan, Nairobi, akijenga hoja kwamba waliotaka kumuua, wangeweza kumfuata Muhimbili.

Ndege ya kukodi ilipatikana. Mbowe alikumbatia mtungi wa gesi kuhakikisha Lissu anapata oksijeni na uhai wake unakuwa kwenye mkondo salama. Alute anapomtambua Mbowe kuwa ndugu yao, ni mwanafamilia wao, ana haki kabisa.

Anayeshiriki kuokoa maisha yako, huyo ni nduguyo. Mbowe siyo tu alishiriki, alipigania uhai wa Lissu. Anayeweka akiba uhai wake kwa ajili ya kutanguliza wa mwenzake, huyo anakuwa anafanya matendo ya kimungu. Mbowe siyo tu alidhihirisha undugu wake kwa Lissu, bali pia aliyathibitisha matendo ya kimungu ndani ya umbo la binadamu.

Vyovyote vile, ungedhani kuwa Mbowe alichora mhuri wa dhahabu kwenye moyo wa Lissu, hivyo asingesahaulika kwenye maisha yake, kutokana na matendo mema aliyomtendea kuokoa uhai wake. Ungedhani, usingetokea wakati kuona Lissu na Mbowe wakitofautiana. Kwamba, nyakati zote, zile siku 122 za kutoka Septemba 7, 2017 mpaka Januari 6, 2018, zingewakumbusha.

Unaweza pia ukastaajabu, jinsi Lissu alivyokuwa akijipiga kifua mbele kumsemea mema Mbowe, au hata kuwarudi waliokuwa wameanzisha vuguvugu dhidi ya Mbowe, ndani ya Chadema au nje, mbona kumekuwa na ukengeukaji mkubwa? Je, vita ya uenyekiti Chadema ina nguvu kuliko undugu au inafuta hadi mhuri wa dhahabu moyoni?

Gwiji wa siasa za Canada na Waziri Mkuu kwa vipindi vingi zaidi nusu ya kwanza ya Karne ya 20, William King, alipata kuandika kanuni kuhusu wanasiasa na vyama vyao, kuwa; “Chama changu cha siasa siyo dini yangu na hakipaswi kuwa dini yako pia.” Chini yake aliweka mwongozo wenye sehemu tatu kwa wanasiasa kuhusu vyama vyao.

Mosi; Chama changu cha siasa siyo mwokozi wangu. Wakristo huamini uwepo wa mwokozi ambaye ni Masiha. King anataka wanasiasa wasivichukulie vyama vyao sawa na Yesu Masiha kwa Wakristo.

Pili; chama changu cha siasa hakinipendi. Hili ni darasa kuwa hakuna chama cha siasa chenye kumpenda mtu. Vyama huhitaji watu ili vijijenge kuwa vikubwa, lakini pale inapobidi chama kinaweza kumjeruhi yeyote kwa ajili ya kutimiza malengo yake.

Tatu; chama changu hakina uzima wa milele. Hakuna chama ambacho kinatoa uhakika wa uzima wa milele kwa mwanachama wake. Hivyo, kila mtu kwenye chama ni wa kupita, leo upo kesho haupo. Hayupo ambaye uhai wake utarefushwa na chama chake.

Mwongozo huo wa King ukiuzingatia vema, hutashangaa kwa nini Mbowe na Lissu wamefika hapa walipo. Kama chama hakipendi watu, basi wanachama au viongozi wa kisiasa hawapendani, isipokuwa hukenuliana meno kwa sababu za kimaslahi.

Unaweza kuwa tayari kupokea risasi leo kwa ajili ya kumwokoa mwanasiasa mwenzako, lakini kesho uliyekuwa tayari kuhatarisha uhai wako kwa ajili yake, akakuning’iniza kwenye msalaba wenye mateso makali. Inawezekana pia, aliyekuokoa leo, kesho akaongoza kusulubishwa kwako.

Leo, pengine muda huu, yupo mtu anateseka kuona uhusiano wa Mbowe na Lissu ulivyovurugika. Hana amani, hapati usingizi. Alipenda kuwaona wakiwa pamoja na aliamini kwamba wanasiasa hao ni imara wakiwa pamoja. Shangaa, wahusika wenyewe kama vile hawajali.

Hatuachi kujikumbusha kuwa kwenye siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu, ila kuna masilahi ya pamoja.

Mbowe na Lissu ni wanasiasa na masilahi yao yapo kisiasa. Juzi, walikuwa marafiki, leo wanakaangana. Kilichowaunganisha ndicho kinawatenganisha. Pengine kitawaunganisha tena mbele ya safari.

Muhimu, kwenye siasa hakuna undugu.

Hili ni funzo kwa kijana ambaye ndiye yupo kwenye kundi lililo na idadi pana ya watu wenye deni kubwa la kuishi, hupaswa kufahamu kuwa kadi ya uanachama haitoi oksijeni, hivyo wanapoielekea siasa lolote linaweza kutokea kwenye vyama vyao, ama kutimuliwa au kuhama. Vilevile, wanaowapenda wakatofautiana. Ukiwa bendera fuata upepo, utapotea mapema.

Katika vyama inaweza pia kutokea kukimbiwa na watu ambao inaaminika ndiyo uhai wa chama au kuwa na viongozi ambao hukubaliani nao mitazamo, kiasi cha kujikuta unakuwa huna furaha. Ukifika hapo kumbuka mambo manne; chama cha siasa siyo dini wala mwokozi, hakina uzima wa milele na hakimpendi mtu. Kwenye siasa hakuna undugu.

Related Posts