Wajipanga hivi kukabiliana na kipindupindu shule zikifunguliwa

Mbeya. Wakati Jiji la Mbeya likieleza hatua za haraka kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu, Kyela nayo imeweka mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo kabla ya shule kufunguliwa.

Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa 23 nchini iliyotajwa na Wizara ya Afya kuwa na mlipuko wa kipindupindu, huku Halmashauri tatu zikitajwa kukumbwa na ugonjwa huo.

Katika Wilaya hizo, Jiji la Mbeya ndilo limetajwa kuwa kinara, Chunya na Mbeya DC, huku hatua za haraka zikiendelea kuchukuliwa kabla ya shule kufunguliwa Januari 13 wiki ijayo.

Takwimu zilizotolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji hilo jana kwenye kikao cha kujadili mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo, Dk Yesaya Mwasubila amesema hadi Januri 6, walihudumia wagonjwa takribani 261.

“Jiji la Mbeya ni miongoni mwa Halmashauri zilizoathiriwa na ugonjwa huu na tangu Desemba hadi Januari 6, tumehudumia wagonjwa 261,” amesema Dk Mwasubila.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Florah Angelo amesema licha ya wilaya hiyo kutokuwa na ugonjwa huo, lakini wamejipanga kudhibiti maeneo yote haswa shuleni.

“Nimeitisha kikao Ijumaa na wakuu wa shule zote, watendaji na watalaamu wa afya, kuhakikisha shule zote zinakuwa na vitakasa mikono, madarasa na madawati ya kutosheleza yapo”

“Darasa la Kwanza bado wanaendelea kujiandikisha na kwa kidato cha kwanza tunatarajia zaidi ya 6,000 japokuwa sina takwimu nzuri labda nijiridhishe zaidi,” amesema Florah.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya DC, Gidion Mapunda amesema hadi sasa wagonjwa ni watano na kifo ni kimoja na kwamba tayari wametenga maeneo maalumu kwa ajili ya wagonjwa hao.

Kuhusu maeneo ya shuleni, kiongozi huyo amesema watazuia biashara ya vyakula badala yake chakula kitatolewa shuleni hapo na huduma ya maji ya moto yatakuwapo kwa ajili ya wanafunzi.

“Tangu kuanza Januari hatuna kifo kingine zaidi ya kile kilichoripotiwa, tumetenga vituo vya afya Ikukwa, Mjele, Mbalizi na Inyala na maeneo yenye mlipuko ni Nsalala, Utengule na Mji mdogo wa Mbalizi,” amesema na kuongeza;

“Tutakaa kikao kikubwa Ijumaa watendaji wote kujadili hatua ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huu na tumejipanga, shule zote lazima ziwe na maji bahati nzuri tuna ziada ya madarasa takribani 89 na upande wa vyoo hatuna changamoto.”

Ofisa Elimu Sekondari Jiji la Mbeya, Batilda Luvanda amesema kutokana na mlipuko huo, tayari wamejipanga kuhakikisha shule zinapofunguliwa miundombinu inakuwa rafiki kwa wanafunzi.

“Tunatarajia wanafunzi 11,914 kujiunga na kidato cha kwanza, miundombinu ipo tayari na tutakuwa na kikao Alhamisi na wakuu wa shule zote na wasaidizi wao, wataalamu wa afya kujadili namna ya kukabiliana na ugonjwa huu,” amesema.

Amesema wanataka wanafunzi wasishikane mikono, lakini kuwepo kwa ndoo za maji ili kila muda wanafunzi wanawe mikono kwa maji tiririka kama ilivyokuwa kipindi cha Uviko – 19.

Related Posts