Zanzibar waitumia Muhimbili kioo utoaji huduma mfumo wa bima

Dar es Salaam. Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Ustawi wa Jamii wameitaja Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kama darasa la utoaji wa huduma za dharura kwa kutumia Mifuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Wamesema Zanzibar ni mwaka mmoja sasa imeanza kutoa huduma kwa kutumia bima ya afya na Hospitali ya Muhimbili imekuwa na uzoefu katika utoaji huduma kwa kutumia bima ya afya kwa zaidi ya miaka 20.

Akizungumza mara baada ya kutembelea hospitali hiyo akiambatana na wajumbe wenzake, leo Jumatano, Januari 8, 2025 Mwenyekiti wa kamati na sheria ndogo ya baraza hilo, Mihayo Juma Nunga amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia namna hospitali hiyo inavyotoa huduma za afya kwa kutumia bima.

“Hospitali hii inauzoefu wa zaidi ya miaka 20 ikitumia bima, tumepita kila eneo kuangalia namna wagonjwa wanavyohudumiwa kwa njia ya bima, eneo la wagonjwa wa dharura wenzetu wapo mbali,” amesema.

“Tutakavyorudi Zanzibar Hospitali ya Mnazi mmoja na Lumumba tutashauri namna wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kwa kutumia bima ya afya,” amesema.

Nunga amesema Hospitali ya Muhimbili itaendelea kuwa ya rufaa kwa Zanzibar hadi watakapoboresha huduma za afya visiwani humo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar, Mbarouk Omary Mohamed amesema bima ya afya kwa upande wa Zanzibar wamekuwa na ushirikiano wa uboreshaji huduma na bima ya afya ya NHIF.

“Tumejifunza namna bima ya afya inavyoshirikiana na hospitali hapa nchini, tumeona Muhimbili ndio kioo cha utoaji huduma ndio maana tumefika na kuangalia ili nasi tukaboreshe huduma zetu,” amesema.

Meneja wa NHIF mkoa wa Ilala, Aifenda Mramba amesema mfuko wa Taifa wa afya Zanzibar wameingia makubaliano na NHIF kutumia mifumo ya mfuko huo katika utoaji wa huduma.

“Viongozi hawa wamekuja kujifunza wapi tulipotoka, tulipo na tunapokwenda na tumeingia nao ushirikiano katika utoaji wa huduma,” amesema.

Akizungumzia maboresho yanayofanyika hospitalini hapo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Rachel Mhavile amesema hospitali hiyo imekuwa ikiboresha huduma pamoja na mazingira ya kazi.

Mtaalamu huyo amesema mbali na huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo wako kwenye mpango wa kujenga upya hospitali hiyo huduma zitolewe katika eneo moja.

Related Posts

en English sw Swahili