Chama karudi, taabu iko palepale

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama aliyekuwa nje akiuguza majeraha, amerudi na alfajiri ya leo ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa kwenye msafara wa timu hiyo ulioenda Mauritania kuwahi pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal, huku kocha Sead Ramovic akiacha wachezaji watatu jijini Dar es Salaam.

Yanga itarudiana na Al Hilal nchini humo inayotumia nchi hiyo kama nyumbani baada ya awali kulala mabao 2-0 hapa nyumbani, lakini ikichagizwa na mzuka wa ushindi wa mabao 3-1 ilioupata mbele ya TP Mazembe ya DR Congo na kufufua tumaini la kutinga robo fainali ya michuano hiyo kutoka Kundi A.

Chama aliyeanza kufanya mazoezi na wenzake mapema ni kati ya wachezaji waliotarajiwa kuwa katika msafara wa timu hiyo, huku Maxi Nzengeli, Yao Kouassi na Aziz Andambwile wakiachwa Dar es Salaam kutokana na hali zao kiafya wakisubiri pambano la mwisho la kundi hilo dhidi ya MC Alger ya Algeria.

Chama, aliyetua Jangwani msimu huu akitokea Simba, alikosekana katika mechi tano zilizopita ikiwamo moja ya kimataifa dhidi ya Mazembe, Yanga iliposhinda 3-1 na akizikosa nne za Ligi Kuu, huku Yao hadi sasa hajacheza mechi tatu za ligi dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Fountain Gate na ile ya TP Mazembe.

Kwa upande wa Nzengeli aliyepata majeraha katika mechi ya ugenini dhidi ya TP Mazembe iliyoisha kwa sare ya 1-1, akikosa mechi tano zikiwamo nne za Ligi Kuu na moja ya kimataifa Yanga ilipowafunga Wakongomani hao 3-1, huku Andambwile aliyeumia wakati wa mechi ya Tabora United ambapo Yanga ililala 3-1 na kukosa mechi saba zilizopita, zikiwamo nne za kimataifa na tatu za Ligi Kuu ambaye alipata majeraha katika mechi dhidi ya Tabora United ambapo Yanga walifungwa mabao 3-1, huku akikosa mechi tisa zikiwamo nne za kimataifa na tano za ligi dhidi ya Namungo, Mashujaa, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Fountain Gate.

Kurejea kwa Chama mwenye rekodi za kusisimua katika michuano ya CAF akiwa na mabao 23 tangu 2017, kunakiongezea nguvu kikosi cha Ramovic kinachohitaji ushindi dhidi ya Al Hilal ili kujiweka pazuri katika kundi hilo kwani kwa sasa ina pointi nne, nyuma ya MC Alger yenye tano, huku Mazembe ikiwa na mbili wakati Al Hilal ikiongoza ikiwa na pointi 10 na ikijihakikisha kwenda robo fainali hadi sasa.

Yanga ikimalizana na Al Hilal itarudi nyumbani Januari 18 kuvaana na MC Alger ambayo wikiendi hii itakuwa nyumbani kuvaana na Mazembe. Katika mechi ya kwanza Yanga ilipasuliwa 2-0 jijini Algers, Algeria.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Chama, habari kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa katika kuhakikisha inaweka mambo sawa kabla ya kuvaana na Al Hilal, imewatanguliza watu wawili Mauritania kucheki mazingira kabla ya timu haijafika nchini humo.

“Kabla ya kikosi kuondoka Dar  alfajiri ya kesho (leo) tayari tumeshajua hali ilivyo ugenini, hivyo alishatangulia Hafidh na kiongozi mmoja wa Kamati ya Mashindano,” kilisema chanzo chetu kutoka Yanga.

Related Posts