DAWA YA KULEVYA AINA YA HEROIN YAADIMIKA, WATUMIAJI WAHAHA

*DCEA yawaonya wafanyabiashara dawa za kulevya, yatoa ombi kwa wananchi

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesema kuwa tathimini ya upatikanaji na usambazaji wa dawa za kulevya inaonesha kuwa, dawa aina ya heroin zimepungua sana hapa nchini.

Akizumgumza na waandishi wa habari leo Januari 9,2025 jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema dawa za kulevya aina ya heroin kwa hapa nchini zimepungua sana kutokana na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa katika kudhibiti dawa za kulevya.

Amefafanua kuwa kupungua kwa heroon kumesababisha idadi kubwa ya waraibu kutumia dawa mbadala kama vile dawa tiba zenye asili ya kulevya na wengine kuhitaji matibabu baada ya kukosa dawa za kulevya mtaani.

Pia amesema baadhi ya watu walianza kutengeneza dawa za kulevya zinazofanana na heroin kutokana na kuwepo kwa uhaba wa dawa hiyo na baadhi yao tayari wamewakamata na kusisitiza wanaendelea kufuatilia kwa karibu uwepo wa dawa mpya za kulevya (NPS).

Ametumia nafasi hiyo kueleza pamoja na mafanikio makubwa ambayo Mamlaka hiyo imeyapata katika mwaka 2024 katika kupambana na dawa za kulevya mwaka 2025 wameweka vipaumbelee kadhaa ili kufikia malengo waliyojiwekea.

“Mwaka 2025, vipaumbele vya DCEA vitahusisha kuimarisha zaidi udhibiti wa dawa za kulevya kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia za kisasa kufuatilia mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya .

“Pia utoaji wa elimu kwa umma ili kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na kujiepusha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya na kuendelea kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya kupitia programu za tiba na urekebishaji kupitia vituo vya tiba kwa waathirika vilivyopo nchini.”

Aidha amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawashukuru kwa dhati wadau wote walioshiriki kwa namna mbalimbali katika kufanikisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya, vyombo vyote vya ulinzi na usalama, na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwani mchango wao umechangia kupata mafanikio makubwa.

“Mamlaka inawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga simu bure kupitia namba 119. Taarifa zinazotolewa zitapunguza usambazaji wa dawa za kulevya na kuikinga jamii isijiingize kwenye matumizi ya dawa hizo.

“Vita dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la serikali pekee, bali ni jukumu la kila mtanzania mwenye mapenzi mema kwa Taifa hili. Tukishirikiana, tunaweza kulinda mustakabali wa Taifa letu dhidi ya janga la dawa za kulevya.”

Hata hivyo amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imeendelea kuwabana ikiwemo kuwakamata wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuwafikisha mahakamani na kuongeza baadhi ya wafanyabiashara wa dawa hizo wamekimbia nchi lakini Mamlaka hiyo imesisitiza kokote ambako wamekimbilia watapatikana na hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.









Related Posts