DCEA yakamata kilo milioni 2.3 za dawa za kulevya 2024

Dar es Salaam. Udhibiti uliowezesha kuzuia kusambaa kilo milioni 2.3 za dawa za kulevya umezuia athari ambazo zingejitokeza na kurudisha nyuma ustawi wa Tanzania.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, imekamata kiasi hicho cha dawa mwaka 2024, kikiwa kikubwa kulinganisha na kilo milioni 1.9 zilizokamatwa mwaka 2023.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi, Januari 9, 2025, amesema kiasi hicho ni kikubwa kuwahi kukamatwa nchini.

“Endapo kiasi hiki kingefanikiwa kusambazwa, kingeleta athari kubwa na kurudisha nyuma ustawi wa Taifa letu,” amesema.

Amesema bangi iliyosindikwa ndiyo iliyokamatwa kwa wingi mwaka 2024, ikifuatiwa na methamphetamine, heroini na dawatiba yenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl.

“Kwa mara ya kwanza dawa mpya ya kulevya aina ya 3-4 Methylene-Dioxy-Pyrovalerone (MDVP) ilikamatwa nchini,” amesema.

Lyimo amesema ufanisi wa ukamataji umetokana na operesheni zilizofanyika nchini, ikiwemo katika eneo la Bahari ya Hindi ambako huingizwa kwa kutumia majahazi.

Amesema kati ya Novemba na Desemba, 2024, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, ilikamata methamphetamine na heroini zenye uzito wa kilo 673.2.

Kati ya dawa hizo, amesema kilo 448.3 ziliwahusu raia wanane wa Pakistan waliokamatwa katika Bahari ya Hindi wakiwa wamezificha ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini humo kwa namba B.F.D 16548, na kilo 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi katika Jiji la Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao wameshafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wanakokabiliwa na mashtaka mawili.

Wamesomewa mashtaka hayo leo, Januari 9, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Washtakiwa hao ni Mohamed Hanif (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pehilwam (50) maarufu Tayeb, Immambakshi Kudhabakishi (55), Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45).

Wakili wa Serikali, Titus Aron, amedai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025, akidai katika shtaka la kwanza wanadaiwa kusafirisha kemikali ya kutengenezea dawa za kulevya aina ya methamphetamine, kosa walilotenda Novemba 25, 2024, eneo la Navy lililopo Kigamboni.

Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini, kosa wanalodaiwa kutenda tarehe na eneo la kosa la kwanza.

Kesi imeahirishwa hadi Januari 22, 2025, itakapotajwa. Washtakiwa wamepelekwa rumande.

Amesema ukamataji wa dawa za kulevya umeendana na utoaji wa elimu kuhusu madhara yake, kuimarisha huduma za matibabu ya waraibu kwa kuongeza vituo vya huduma za tiba na utengemao na kuimarisha ushirikiano na wadau ndani na nje ya nchi.

Lyimo amesema kwa mwaka 2024, mamlaka kwa kushirikiana na taasisi nyingine walitoa elimu kwa watu 28 milioni kuhusu madhara ya dawa hizo.

Katika kupanua huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini, DCEA kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo imeongeza vituo viwili vya matibabu mkoani Pwani na Dar es Salaam, hivyo kuwa na jumla ya vituo 18.

“Vituo hivi 18 vinahudumia waraibu 18,170 kwa kutoa huduma za utengemao kwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya afyuni kama vile heroini na baadhi ya dawatiba zenye asili ya kulevya kama Tramadol na Pethidine,” amesema.

Amesema wameongeza nyumba sita za upataji nafuu (Sober House) na kufikia 62 ambazo zinatoa huduma kwa waraibu 17,230.

“Waraibu wengine wa dawa za kulevya na vilevi vingine zaidi ya 900,000 walihudumiwa katika vitengo vya afya ya akili vilivyopo kwenye hospitali za wilaya, mikoa na hospitali za rufaa za kanda,” amesema.

Amesema tathmini ya upatikanaji na usambazaji wa dawa za kulevya inaonyesha heroini zimepungua nchini, hali iliyosababisha idadi kubwa ya waraibu kutumia dawa mbadala kama vile dawatiba zenye asili ya kulevya na wengine kuhitaji matibabu baada ya kukosa dawa za kulevya mtaani.

“Vilevile, baadhi ya watu walianza kutengeneza dawa za kulevya zinazofanana na heroini,” amesema.

Related Posts