Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, iliyopo Kinondoni imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya jaribio la kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo.
Kesi inayowakabili mjasiriamali, Fredrick Said na wenzake watano ilikuwa imepangwa leo Alhamisi, Januari 9, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, kwa washtakiwa wangesomewa maelezo ya awali ya kesi na kisha usikilizwaji kamili, yaani Mahakama kuanza kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo, mahakama hiyo haikuweza kuendelea kutokana na jalada la kesi kutokuwepo.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Daisy Makakala ameieleza mahakama kesi hiyo haiwezi kuendelea kwa kuwa hakuwa na jalada, huku akifafanua liliitwa Dodoma (Makao makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka – NPS).
“Shauri hili lilikuja kwa ajili ya hoja za awali lakini hatuko tayari kwa kuwa sina jalada halisi na kwa taarifa nilizonazo ni kwamba lilikuwa Dodoma lakini liko njiani linakuja. Hivyo tunaomba tupangiwe tarehe nyingine,” amesema Wakili Makakala.
Hoja hiyo haikupingwa na washtakiwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila ameahirisha kesi hiyo mpaka Januari 21, 2025 kwa ajili ya kuendelea na hatua hizo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemarila anayesikiliza kesi hiyo ameahirisha hadi Januari 21, mwaka huu kwa ajili ya hatua hizo.
Hii ni mara ya pili mfululizo kukwama. Mara ya kwanza ilipangwa kusikilizwa katika hatua ya awali na kisha kuendelea na ushahidi Desemba 19, 2024.
Siku hiyo haikuendelea na Wakili Makakala aliieleza Mahakama walikuwa hawajakamilisha kuandaa maelezo hayo ya awali ya kesi.
Hivyo Wakili Makakala aliomba Mahakama ipange tarehe nyingine ndipo Hakimu Rugemarila akaipanga leo.
Mbali na Fredrick, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Isack Mwaifani, Benki Mwakalebela ambaye ni wakala Stendi ya Magufuli, Bato Bahati Tweve, Nelson Elimusa ambaye dereva wa teksi na Anita Temba.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kujaribu kuteka mtu na kumuweka kizuizini isivyo halali kinyume na vifungu vya 380(1) na 381(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa shtaka hilo, Desemba 6, 2024.
Mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali John Mwakifuna alidai kuwa Novemba 11, 2024, katika eneo la Kiluvya Madukani Lingwenye, jijini Dar es Salaam washtakiwa hao walijaribu kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo kwa nia ya kumuweka kizuizini isivyo halali.
Washtakiwa wote walikana shtaka hilo na Wakili Mwakifuna akaieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa umekamilika na akaomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Hata hivyo, Hakimu Rugemalira alipanga tarehe hiyo kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (washtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi) pamoja na usikilizwaji kamilii, Mahakama kuanza kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka.
Washtakiwa watano kati yao wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana isipokuwa mmoja ambaye bado hajatimiza masharti hayo.
Masharti hayo ya dhamana ni kila mmoja kusaini bondi ya dhamana ya Sh10 milioni, kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka kwa waajiri wao kama ni waajiriwa, au kutoka mtendaji wa kata wanakoishi na kutokutoka nje ya mkoa bila ruhusa ya Mahakama.