Dar es Salaam. Zikiwa zimepita wiki tatu tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), Baraza Kuu la Uongozi limewachagua viongozi wapya wa sekretarieti ya chama hicho watakaohudumu kwa miaka mitano ijayo.
Katika mkutano mkuu wa CUF uliofanyika Desemba 18, 2024, Profesa Ibrahim Lipumba alichaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa chama hicho, akiwa tayari amekiongoza kwa miaka 25.
Profesa Lipumba aliukwaa wadhifa huo baada ya kupata kura 216 katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho, akiwashinda wenzake saba waliokuwa wakichuana naye katika nafasi hiyo, huku wengine wakichaguliwa katika nafasi nyingine.
Aliyemfuatia Profesa Lipumba katika uchaguzi huo ni Hamad Masoud Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, ambaye alipata kura 181.
Aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CUF bara, Maftah Nachuma aliyefuatia katika nafasi ya tatu akipata kura 102, huku Wilfred Rwakatare akipata 78. Wengine ni Juma Nkumbi aliyepata kura sita, Athumani Kanali kura tano, Chifu Yema na Nkunyuntila Chiwale wakiambulia kura mbili kila mmoja.
Katika nafasi ya makamu mwenyekiti (Tanzania Bara), Othman Dunga aliibuka mshindi huku Mbarouk Seif Salim akiibuka mshindi katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Zanzibar).
Kutokana na ushindi huo, Profesa Lipumba alipata fursa ya kupendekeza majina ya viongozi wa sekretarieti mpya ambao walipigiwa kura za “ndiyo” au “hapana” na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF.
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa chama hicho Mashaka Ngole, waliochaguliwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF ni Husna Mohamed Abdallah ambaye ndiye Katibu Mkuu mpya baada ya kupata kura 19 dhidi ya kura 11 alizopata Ali Abarani.
Ngole ameeleza kwamba katika uchaguzi huo, kura tano ziliharibika na wajumbe 10 walikuwa wameondoka kikaoni, hivyo hawakupiga kura.
Amesema kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya ameshinda kwa kupata kura 29 za ‘ndiyo’, huku Ali Juma Hamisi akishinda nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar kwa kura 41 za ‘ndio’ kati ya kura 45.
Husna amechukua nafasi ya Hamad ambaye alichaguliwa kushika nafasi hiyo Machi 25, 2022, akitokea ACT Wazalendo alikokwenda baada ya kuhama CUF na kurejea tena, kisha kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu.
Katika safu hiyo ya sekretarieti ni Sakaya pekee ndiye ameendelea kubakia kwenye nafasi yake, huku wengine wote wakiwa wapya.
Husna, ambaye ndiyo Katibu Mkuu wa kwanza mwanamke wa CUF, alizaliwa Januari 11, 1983 huko Pemba, Zanzibar na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Kidongo Chekundu kati ya mwaka 1990 – 1997.
Mwaka 1998 hadi 2002, alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Uweleni na baadaye kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Lumumba kati ya mwaka 2003 – 2005.
Husna alijiunga na chuo cha ualimu cha Nkurumah kuanzia mwaka 2004 hadi 2006. Baadaye mwaka 2013 – 2017, alisoma shahada ya ugavi na manunuzi katika Chuo cha Usimamizi wa Biashara (CBE).
Ana uzoefu wa kazi ya ualimu ambayo aliifanya kati ya mwaka 2006 – 2008 katika Shule ya Sekondari ya Mwembeladu iliyopo Zanzibar. Mwaka 2008 alihamia Shule ya Mawelewele iliyopo mkoani Iringa na baadaye mwaka 2009 hadi 2016, alifundisha Shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege iliyopo Dodoma.
Nafasi za kisiasa alizowahi kushika ni pamoja na mjumbe wa kamati ya uongozi Jimbo la Welezo, katibu wa aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho kabla ya kuhamia ACT Wazalendo, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, mjumbe wa mkutano mkuu wa chama taifa na mgombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi jana, Husna ameeleza malengo yake kuwa ni pamoja na kukirudisha chama hicho katika hali yake ya awali kwa sababu kimepitia misukosuko mingi.
“Jambo la kwanza ninalokwenda kulisimamia ni kuondoa hitilafu zilizopo kwa sababu mahali popote penye mkusanyiko wa watu, hapakosi hitilafu, watu wote wawe na dhamira moja,” amesema.
Husna amesema anakusudia pia kuhakikisha kwamba chama hicho kinapata ushindi kwenye uchaguzi wa 2025. Aliongeza kwamba atakwenda kupaza sauti kuhakikisha Watanzania wanapata Katiba mpya.
Akizungumzia matarajio yake kama kada wa CUF, Salehe Mahimbo amesema anatarajia kuona sekretarieti mpya ikisimamia suala la kupatikana kwa Katiba mpya pamoja na tume huru ya uchaguzi wanayoitaka.
“Hata ukiwa na sekretarieti nzuri kiasi gani, kama hatuna Katiba mpya na tume ya uchaguzi tuitakayo, hatuwezi kufikia malengo yetu ya kushika dola.
“Baraza Kuu wamemchagua Katibu Mkuu mpya, tena ni mwanamke. Wanawake wanasikilizwa, tena Rais tuliyenaye ni mwanamke. Kwa hiyo, atumie fursa hiyo kupata mambo ambayo tunayahitaji,” amesema Mahimbo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana (Juvicuf) Temeke.
Kwa upande wake, Mwinyi Bakari alisema sasa ni wakati wa kuwapa ushirikiano viongozi waliochaguliwa ili kwa pamoja wapiganie malengo ya chama chao hasa mwaka huu wa uchaguzi.
“Wanachama na viongozi tukishirikiana kwa umoja, tutapata Katiba mpya na mambo mengine ambayo tumekuwa tukiyapigania kila siku. Tusiwaache viongozi peke yao, mapambano haya yanatuhitaji sote,” amesema kada huyo wa CUF.
Jukumu la kukifufua chama
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema lengo la chama chochote ni kushika dola, hivyo ni lazima katibu mkuu mpya apambane kuhakikisha chama hicho kinafikia lengo hilo.
Pia, amesema CUF kimefifia kwenye siasa za Tanzania kwa sasa, hivyo ana jukumu la kuhakikisha anakifufua, kukiaminisha kwa wananchi na kupata wanachama wapya ili kiendelee kuwa kwenye ramani.
“CUF imeyumba baada ya kuja kwa ACT Wazalendo, hivyo viongozi wa chama hicho wana kazi kubwa ya kuwashawishi wananchi ili wakichague katika nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema mwanazuoni huyo.
Amesisitiza kwamba chama hicho kina jukumu la kujenga hoja zenye nguvu ili kukabiliana na chama tawala cha CCM ambacho kiko imara na kina nguvu na ufuasi mkubwa kuliko vyama vingine vya upinzani nchini.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza amesema chama hicho kinahitaji kujiimarisha zaidi ili kirudishe imani ya wananchi ambayo imekuwa ikipotea mwaka hadi mwaka.
“Migogoro ndani ya chama pia inasababisha vyama kupoteza mvuto, ni wakati sasa wajifunze kwa yaliyotokea huko nyuma ili waendelee kuwa imara. Uongozi unahitaji busara wakati wa kufanya uamuzi,” amesema.