Kisiwa cha Bawe ni kisiwa kidogo kilichopo umbali wa takriban kilomita 10 kutoka Stone Town, Zanzibar. Kisiwa hiki kina historia ndefu, ambapo mwishoni mwa karne ya 18, Sultan Barghash ibn Sa’id alikitoa kwa kampuni ya Eastern Telegraph, iliyokitumia kama kituo cha uendeshaji wa waya wa chini ya bahari unaounganisha Zanzibar na Shelisheli na Aden.
Mkataba huo uliongezwa na Sultan Khalifa ibn Sa’id mwaka 1889 kwa faida ya kampuni ya Cable & Wireless, ambayo ilijenga nyumba kwenye kisiwa hicho kuwahudumia wafanyakazi wao.
Hivi karibuni, Kisiwa cha Bawe kimepata umaarufu mpya baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kufungua rasmi hoteli ya kitalii ya Bawe Island by Cocoon Collection tarehe 7 Januari 2025. Katika hafla hiyo, Rais Samia aliunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kuhusu umuhimu wa wawekezaji kutumia fursa walizopewa kwa wakati, akisisitiza kuwa visiwa ambavyo havijaendelezwa vitarejeshwa serikalini ili wapewe wawekezaji wenye uwezo.