Dar es Salaam. Vita ya kukabiliana na dawa za kulevya zinazoathiri nguvu kazi ya Taifa hasa vijana, imeendelea kushika kasi na sasa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiania na vyombo vingine vya usalama, imekamata dawa za kulevya aina ya methamphetamine na heroin zenye uzito wa kilo 673.2.
Kati ya dawa hizo, kilo 448.3 ziliwahusisha raia wanane wa Pakistani waliokamatwa katika Bahari ya Hindi, zikiwa zimefichwa ndani ya jahazi lililosajiliwa nchini Pakistani kwa namba B.F.D 16548.
Pia, kilo 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi katika Jiji la Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi Januari 9, 2025 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tathmini ya dawa kulevya zilizokamatwa kwa kipindi cha mwaka 2024.
Lyimo amesema kiasi hicho cha dawa kimekamatwa kati ya Novemba na Desemba, mwaka 2024.
“Tulipowahoji raia hawa wa Pakistani walisema wamekuwa wakifanya biashara hii ya kusafirisha dawa za kulevya kwa kipindi cha miaka 28 kutoka Bara la Asia kuja Afrika na wanapozifikisha Afrika, huzisambaza kwenye nchini ambazo nyingine kwa kutumia majahazi au usafiri mwingine kama nchi hizo hazipakani na bahari” amesema Lyimo na kuongeza:
“Jahazi hili tulilolikamata lina uwezo wa kupakia tani nane za dawa za kulevya na kwamba kukamatwa kwa jahazi hili kumekata mnyororo,” ameongeza.
Hata hivyo, amesema raia hao wa Pakistani watafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya hatua za kisheria, muda wowote leo.
Endelea kufuatilia Mwananchi