Kilimanjaro Stars yamaliza Mapinduzi Cup bila bao, pointi

KATI ya timu nne zilizoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025, ni Kilimanjaro Stars pekee ambayo haijafunga bao wala kupata pointi baada ya mechi tatu.

Kilimanjaro Stars inayoundwa na wachezaji kutoka Tanzania Bara, leo Januari 9, 2025 imepoteza mchezo wa tatu kwa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso ambayo imejikatia tiketi ya kucheza fainali ikifikisha pointi saba.

Kipigo hicho kwa Kilimanjaro Stars kimefuatia baada ya kuanza kufungwa 1-0 dhidi ya Zanzibar Heroes kisha 2-0 mbele ya Kenya.

Katika mchezo wa leo uliochezwa Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba, Burkina Faso ilipata mabao yake yote kipindi cha kwanza kupitia Abdoulkarim Baguian dakika ya 30 na Clement Pitroipa dakika ya 41.

Kocha wa Kilimanjaro Stars, Ahmad Ally katika mchezo wa leo alifanya mabadiliko makubwa ya kikosi kulinganisha na mechi zilizopita akitoa nafasi kubwa kwa wachezaji wengine akiwemo kipa Ramadhan Chalamanda ambaye amedaka kwa mara ya kwanza.

Wengine waliopewa nafasi ya kuanza leo ni Vedastus Masinde, Wilson Nangu, Said Naushad, Joshua Ibrahim na William Edgar.

Wakati Kilimanjaro Stars ikiumaliza mwendo huku Burkina Faso ikitangulia fainali, kesho Januari 10, 2025 ni zamu ya Zanzibar Heroes kuikabili Kenya.

Mchezo huo utatoa nafasi kwa timu moja kuungana na Burkina Faso kucheza fainali Januari 13, 2025.

Zanzibar Heroes ili icheze fainali lazima iibuke na ushindi utakaoifanya ifikishe pointi sita kutokana na sasa kuwa nazo tatu wakati Kenya ikihitaji sare pekee iwe na pointi tano kutoka nne za sasa kuifuata Burkina Faso.

Saa 1 usiku mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.

Michuano hiyo iliyoanza Januari 3, 2025, Burkina Faso imecheza mechi tatu, ikifunga mabao manne na kuruhusu moja ikikusanya pointi saba kutokana na kushinda mbili na sare moja.

Kilimanjaro Stars katika mechi tatu, imepoteza zote ikiruhusu mabao matano huku yenyewe ikiwa haina bao.

Kenya katika mechi mbili ilizocheza imeshinda moja na sare moja ikiwa na pointi nne ikifunga mabao mawili na kuruhusu moja wakati Zanzibar Heroes mechi zake mbili imeshinda moja na kupoteza moja ikifunga bao moja na kuruhusu moja. Ina pointi tatu.

Related Posts