TIMU ya kikapu ya Kurasini Heat imeifumua Magnet kwa pointi 69-28 katika Ligi Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam, lakini nahodha wa timu hiyo, Dominic Zacharia amesema nguvu yao kwa sasa wameielekeza katika hatua ya robo fainali.
Hayo aliyasema baada ya timu hiyo kushika nafasi ya tatu kwa pointi 25, huku takwimu zinaonyesha endapo itapoteza michezo mitatu iliyobakia, itafikisha pointi 28 itakayoipa nafasi ya timu hiyo kucheza hatua ya robo fainali.
Sheria ya mchezo wa kikapu zinaeleza timu inayofungwa inapewa pointi 1 na iliyoshinda inapewa pointi 2.
Akizungumzia kuhusiana na timu hiyo kwa sasa, alisema ipo pazuri licha ya kuwakilishwa na vijana wengi chipukizi na anaona wakikomaa watafika mbali zaidi.
“Kwa kweli tumejipanga, kurudisha heshima ya timu hiyo, iliyopotea miaka minne iliyopita,” alisema Zacharia.
Katika mchezo mwingine ulichezwa kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini, timu ya Kibada Riders iliifunga Mgulani Heroes kwa pointi 56-34.
Timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza la Mkoa wa Dar es Salaam ni 18, timu tatu zitakazofanya vizuri zitacheza ligi ya BDL mwaka huu.