MRATIBU wa michezo katika kituo cha JMK Youth Park, Bahati Mgunda amesema watoto 120 walishiriki mafunzo ya mchezo wa kikapu kwenye Uwanja wa Shule ya Margery Wolf Kuhn iliyoko wilaya ya Bagamoyo.
Kwa mujibu wa Mgunda, walioshiriki ni watoto wa umri chini ya miaka 16, 14, 12, 8 na 6 kutoka wilaya ya Bagamoyo.
Alisema mafunzo hayo yaliandaliwa na Mambo Basketball kwa kushirikiana na iCARRe Foundation pamoja na Chama cha Kikapu Mkoa Pwani.
Mgunda ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mambo Basketball, alisema katika mafunzo hayo watoto walijifunza jinsi ya kudunda mpira, kutoa pasi pamoja na stadi za maisha.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Pwani, Abdallah Mpogole, aliwapongeza waandaaji kwa kuanda mafunzo kwa watoto hao.
“Kwa mafunzo yalitolewa kwa watoto hao itawafanya waweze kuupenda mchezo huo tangu wakiwa wadogo. Hili ni jambo zuri,” alisema Mpogole.