Mahakama Kuu ilivyopangua adhabu ya mfungwa wa uchawi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imeamuru kuachiliwa huru mara moja kwa mfungwa aliyekuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa linalohusiana na uchawi, Iddy Hussein, kutokana na adhabu hiyo kutokuzingatia misingi ya kisheria katika kutoa adhabu.

Mahakama hiyo imetoa amri hiyo katika hukumu iliyotolewa na Jaji John Nkwabi kufuatia rufaa aliyoikata akipinga adhabu hiyo aliyohukumiwa baada ya kukiri shtaka lililokuwa likimkabili na wenzake.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo mjibu rufaa, Jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Fortunatus Maricha iliunga mkono rufaa hiyo baada ya kukubaliana na baadhi ya sababu za rufaa, kukiri kwake kosa hakukuwa kwa dhahiri.

Hata hivyo, Jaji Nkwabi katika hukumu yake aliyoitoa jana Jumatano, Januari 8, 2024, hakukubaliana na sababu hizo zilizoungwa mkono na Wakili wa Serikali badala yake amemuachilia huru Iddy kwa sababu tofauti.

Katika hukumu hiyo Jaji Nkwabi amekubaliana na hatia lakini akasema walipaswa kuhukumiwa adhabu ya kulipa faini kwamba sababu aliyoitoa hakimu ya kuwafunga ni batili na hivyo hata adhabu hiyo pia ni batili.

Iddy alishtakiwa pamoja na wenzake wawili kwa kosa la kumiliki vifaa vya kichawi, kinyume cha kifungu cha 3 (b) cha Sheria Uchawi, Sura ya 18, Marejeo ya mwaka 2002.

Kwa mujibu wa maelezo ya shtaka na maelezo ya awali ya kesi, Iddy na wenzake  Januari 18, 2024 katika kijiji cha Buhigwe wilayani Buhigwe mkoani Kigoma walikutwa wakimiliki vifaa vya uchawi, ambavyo ni mkuki, kioo na usinge na dawa mbalimbali za asili.

Siku hiyo walikuwa wakisafiri kutoka Kasulu Manyovu, kwa kutumia gari aina ya Toyota Probox na wakiwa katika barabara ya Manyovu Buhigwe, walisimamishwa na askari polisi na ilipokaguliwa walikutwa na vifaa hivyo vya uchawi pamoja na dawa hizo.

Walikamatwa na kupelekwa katuo cha Polisi Buhigwe kwa hatua zaidi za kisheria na baada ya upelelezi kukamilika walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Buhugwe.

Waliposomewa shtaka walikiri kisha wakasomewa maelezo ya awali ya kesi ambayo waliyakubali kuwa ni ya kweli na sahihi.

Hivyo mahakama hiyo iliwatia hatiani kama walivyoshtakiwa kutokana na kukiri kwao kosa na ikawahukumu adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, huku mahakama ikitoa sababu kuwa kuna kukithiri kwa uvunjaji wa amani wilayani Buhigwe unaosababishwa na imani za kichawi.

Hata hivyo, alikata rufaa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma kuipinga hatia na adhabu hiyo, akiwasilisha sababu tano.

Siku ya usikilizwaji warufani, alijiwakilisha mwenyewe wakati Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Fortunatus Maricha, ambaye alikubaliana na sababu za rufaa hususani sababu ya kwanza, ya pili na ya tatu kuwa zina mashiko.

Katika sababu hizo za rufaa ambazo wakili wa Serikali Maricha alikubaliana nazo, zote walieleza hakimu alikosea kuwatia hatiani na kuwahukumu adhabu hiyo kwa kuzingatia kukiri kwao kosa ambako hakukua kwa dhahiri na kwenye utata na kwamba hivyo hukumu hiyo ina makosa.

Wakili Maricha ameieleza Mahakama kuna uwezekano mkubwa hawakufahamu walichokuwa wanakikubali.

Ameeleza kama warufani wangechagua kulipa faini (kwa shtaka lililokuwa likiwakabili) asingepinga.

Hata hivyo, Wakili Maricha alipendekeza kesi yao ianze kusikilizwa upya kwa maelezo kuwa kesi hiyo haikuwa imesikilizwa katika ustahilifu wake kwa sababu kwamba warufani walikubali maelezo yote ambayo yanaunda kosa.

Hata hivyo, Jaji John Nkwabi katika hukumu yake amesema kuwa baada ya kuzingatia hoja za pande zote na msimamo wa kisheria, hakubaliani na hoja za warufani kuwa kukiri kwao hakukuwa kwa dhahiri.

Pia, amesema anashindwa kuelewa madai kuwa hawakufahamu maelezo ya kesi waliyoyakiri kwa kuwa hakuna mahali palipoelezwa kuwa hawakuyafahamu, kwa sababu mwenendo huo uliendeshwa kwa Kiswahili, lugha wanayoifahamu kwani hakuna mahali walikoeleza hawafahamu Kiswahili.

Jaji Nkwabi alihoji kama hawakuelewa maelezo ya kesi kwa nini walikubali maelezo hayo ya kweli na sahihi, huku akisema kwa mtazamo wake madai hawakuyafahamu maelezo hayo.

Hata hivyo amekubaliana na sababu ya rufaa iliyohusiana na adhabu ya kifungo waliyopewa badala ya faini.

Iddy alidai ilikuwa ni mara yao ya kwanza kufanya kosa na kwamba si kweli makosa hayo yamekithiri, ambayo pia iliungwa mkono na Wakili Maricha.

Katika kuamua sababu hiyo, Jaji Nkwabi amerejea msimamo wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake wa kesi kadhaa mshtakiwa anapokuwa mkosaji wa mara ya kwanza msisitizo unapaswa uwe adhabu ya mbadala isipokuwa kama ni kosa kubwa ambalo adhabu kali inahitajika au kama makosa hayo yamekithiri.

Amesema sababu iliyotolewa na mahakama ya chini ya kukithiri kwa makosa hayo na kwamba husabanisha kuvunjika kwa amani katika wilaya hiyo, haipo kwenye mwenendo wa kesi hasa katika maelezo ya awali ya kesi waliyosomewa washtakiwa.

Amesema kuwa badala yake ilielezwa tu na mwendesha mashtaka wakati akielezea kumbukumbu za nyuma za washtakiwa na si katika hatua kutoa adhabu na kwamba hivyo washtakiwa hawakumpata nafasi ya kuizungumzia, kuikubali au kuikataa kama walivyofanya kwenye hatua ya rufaa hiyo.

Jaji Nkwabi amerejea msimamo wa Mahakama ya Rufani kuwa hoja inayoibuliwa na Mahakama bila kuwapa nafasi wadaawa kusikilizwa inakuwa ni batili.

“Kwa sababu adhabu iliyotolewa na mahakama ya awali ilitokana na msingi wa hoja ambayo ni batili, adhabu hii haiwezi kusimamia inapaswa kuingiliwa na Mahakama hii,” amesema Jaji Nkwabi.

Kuhusu hoja ya Wakili Maricha kuamuru kesi kusikilizwa upya, Jaji Nkwabi amesema kuwa amri kama hiyo haiwezi kutolewa kwa kuwa mwenendo wa kesi hiyo haukuwa batili wala kuwa na kasoro za kisheria.

Amesema kwa kuwa adhabu waliyopewa ni batili (kifungo jela), na kwamba kama atatoa adhabu ya faini, muda ambao wamekaa gerezani unapaswa kuzingatiwa.

Hata hivyo amesema kwa kwa mtizamo wake hawezi kubadili adhabu hiyo kuwa faini bali anaamuru adhabu ya kifungo cha miezi 12.

Hivyo amesema kwa kuzingatia warufani wameshakata gerezani wakitumikia kifungo kwa takribani mwaka mzima kwa adhabu hiyo warufani wanapaswa kuachiliwa kutoka gerezani mara moja.

Related Posts