Mashemasi 18 Moshi wapata upadre, Askofu Pengo awafunda

Moshi. Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu Katoliki la Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka mapdre vijana kuwa tayari wakati wowote kwenda  kufanya kazi za kitume  katika vituo vya kazi  wanavyopangiwa.

Mbali na wito huo, Askofu Pengo amewataka pia mapdre hao kuwa mfano mzuri wa kanisa na kutenda sawa sawa na utume wao ili kuondoa malalamiko katika jamii au wanakopangiwa kwenda kutoa huduma.

Askofu Pengo ameyasema hayo leo, Januari 9, 2025 wakati wa Misa takatifu ya upadirisho wa mapdre 18 iliyofanyika katika parokia ya Kristu Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

“Niwaombe mapadre wenzangu umri wa katikati(vijana) muwe tayari kwenda nje ya Jimbo la Moshi kufanya kazi ya Mungu. Unajua mahitaji hayaishi kamwe lakini ndio upadre wetu kwa mfano wa Melkizedeki asiyetambulika na baba yake,”amesema Askofu Pengo.

Pia ameongeza kusema;-“Ukipelekwa Lindi mambo yasiende sawa sawa lawama itarudi jimboni kwanini umetuletea padre kijana ambaye hata wao wenyewe hawajamuona akifanya kazi,  labda amemsukumizia kwetu kwa sababu ni tatizo”.

Akitoa mfano wa utume wake, Askofu Pengo amesema “Nimefurahi kusikia mapdre hawa wapya wanapelekwa hata nje ya Jimbo la Moshi, mimi nilipopata upadre nilikuwa padre wa Jimbo la Sumbawanga na nilikaa kule miaka miwili na baada ya pale sijawahi kufanya kazi jimbo la Sumbawanga kwasababu Askofu wangu aliweza kunituma na nikakaa nje miaka 53 ya upadre”.

Akizungumza katika misa hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Lodovick Minde amewashukuru wazazi kwa namna walivyowalea watoto wao na kufikia hatua ya kupata daraja la upadre.

Askofu Minde amesema mapadre wa kanisa hilo wanasoma sana na kwamba ni lazima walelewe katika mazingira ya sala, sadaka na kupenda elimu.

“Tuwashukuru sana wazazi wa hawa mapadre, asanteni mno kwa kutupa hawa watoto, kwani kama sio ninyi tusingewapata. Kwa hakika asanteni sana kwa malezi mema ya sala, sadaka na kupenda elimu, kwani Mapadre wa katoliki wanasoma sana”

Related Posts