Miaka 10 ya Eyakuze Twaweza: Safari ya milima na mabonde

Dar es Salaam. Baada ya miaka 10 ya milima na mabonde katika ushawishi wa sera na kusikiliza sauti za wananchi, sasa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza East Africa, Aidan Eyakuze anastaafu.

Eyakuze anayestaafu Machi, 2025 anakwenda kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ubia wa Serikali ya Uwazi (OGP) yenye makao makuu nchini Marekani.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi jana Jumatano Januari 8, 2025 jijini Dar es Salaam, Eyakuze amesema safari yake ya miaka 10 ndani ya Twaweza East Africa imejaa milima na mabonde, akisimamia misingi ya taasisi hiyo ambayo ni uwazi, ushirikishwaji wananchi na uwajibikaji.

Mkurugenzi Mtendaji anayemaliza muda wake katika Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa Mwananchi (Hayupo pichani). Picha na Sunday George

Kazi chini ya uongozi wake

Eyakuze anasema katika kipindi cha uongozi wake wametatua changamoto za wananchi kwa kuwasilisha sauti zao.

 “Kabla sijajiunga na Twaweza walikuwa wameanzisha Mradi wa Sauti za wananchi ambao tunawahoji kuhusu uelewa wa mambo tofauti, masuala ya kiuchumi, kipato na elimu.

“Baada tu ya kuanzisha hilo, Serikali ya Jakaya Kikwete (Rais awamu ya nne) ikapitisha bajeti ambayo ilitaka itoze kodi ya kadi za simu ya Sh1,000,” anasema.

“Tukaenda kwa wananchi tukawahoji, wananchi wakasema hii ina utata, ndipo ikabadilishwa kutoka kwenye kodi ikawa excise duty (ushuru wa bidhaa) kwenye muda wa maongezi, ambayo ikawa na usawa zaidi, haimuumizi mwananchi wa chini au kumpendelea wa juu,” anasema Eyakuze.

Anasema utafiti kama huo waliurejea mwaka 2022 baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kuja na tozo ya miamala ya simu.

“Tukaenda tukawauliza wananchi, mnaionaje hii kodi, ilikuwa Agosti, 2022. Serikali na mawaziri wakasikiliza wakaanza kujieleza kwa nini tunafanya kitu hiki, lakini baada ya muda, ilipofika Oktoba, 2022 ikapunguzwa.

“Kwa hiyo, naona ni ishara kwamba, kazi zetu zimepaza sauti za wananchi wa kawaida kabisa wakaishawishi Serikali kubadilisha sera,” anasema.

Katika kipindi chake, Eyakuze ambaye ni mchumi kitaaluma, anasema taasisi ilibuni mfumo wa kuwapa motisha walimu ambao wanafunzi wao wanafaulu katika stadi za msingi kama vile kusoma, kuandika na kuhesabu.

“Tunachokifanya ni kuwapa ahadi walimu wakati shule zinafunguliwa. Awali, tulianza na shule 100 na sasa tumechukua shule 265 kwenye mikoa 10 ambayo ina changamoto lubwa ya elimu, tofauti na mikoa kama Dar es Salaam na Kilimanjaro ambako angalau miundombinu ya elimu msingi haina shida sana.

“Hatuwapi mafunzo, nyezo zaidi, vitendea kazi hapana. Tunawaambia wanafunzi wako wakifaulu katika stadi hizi, utapata motisha hii ambayo ni fedha taslimu,” anasema.

Mbali na hayo, Eyakuze anasema walitafuta maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba na matokeo yake wameyapeleka kwenye mchakato wa kutengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Ndiyo maana ukisoma Dira, msingi wake ni utawala bora, usalama, amani na utulivu, kwa sababu wananchi walisema hayo ni muhimu,” anasema Eyakuze ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya maandalizi ya dira hiyo.

Eyakuze amewahi kutajwa kuwa miongoni mwa watu 50 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani waliofanya mapinduzi katika Serikali na Apolitical na World Economic Forum mwaka 2021.

Akielezea hatua hiyo, anasema kutambuliwa huko kulitokana na ubunifu uliofanywa na Twaweza wa kutoa simu kwa wananchi kwa ajili ya kupata maoni yao.

“Tulibuni kitu ambacho kinatumiwa na Benki ya Dunia (WB) na kinatumika kwa nchi nyingine. Wakasema huu ni ubunifu wa taasisi ambao una ushawishi katika nchi nyingine,” anasema.

Eyakuze aliyejiunga na Twaweza East Africa mwaka 2015, anasema moja ya changamoto alizokumbana nazo ni mabadiliko ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO) mwaka 2019. 

“Hata hapa, Tanzania tumepitia vikwazo kwa sababu tulikuwa tumejisajili kwa Sheria ya Kampuni ya mwaka 2019 na ikabidi tujisajili kwa Sheria ya Mashirika yasiyo ya kiserikali,” anasema huku akieleza misimamo tofauti ya nchi inavyoyumbisha malengo ya taasisi hiyo.

“Twaweza iko Kenya na Uganda, unaweza kukuta Serikali zinachukua msimamo tofauti kuhusu asasi za kiraia,” anasema.

Kutokana na madiliko ya sheria hizo, Eyakuze anasema asasi za kiraia zinakosa uhuru wa kufanya kazi zake.

Mkurugenzi Mtendaji anayemaliza muda wake katika Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa Mwananchi. Picha na Sunday George

“Ukisema sana mambo au ukifanya kitu kikaonekana hauendi na mwenendo fulani wa wanaoupenda au ukiwa unakaza sauti sana, unaweza kuingiliwa na sheria zinaruhusu.

“Kuna Sheria ya Makosa ya Mtandao, kuna sheria ya NGO na nyinginezo zinazoruhusu Serikali kuingilia au kukudhibiti,” anasema.

Utafiti uliomweka matatani

Anasema mwaka 2018 hadi 2020 ilikuwa yenye changamoto kwake baada ya Idara ya Uhamiaji kumnyang’anya pasi ya kusafiria kutokana na wasiwasi kuhusu uraia wake.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya kutoa matokeo ya utafiti ambao pamoja na mambo mengine, ulionyesha kushuka kwa umaarufu wa hayati Rais John Magufuli.

“Kazi yangu inanihitaji nisafiri kwenye ofisi za Kenya na Uganda, kwa hiyo kwa karibu miaka mitatu sikuweza kusafiri nje ya Tanzania. Ikaniwia vigumu kufanya kazi,” anasema.

Anasema mwaka 2020 yalipotangazwa maambukizi ya Uviko-19 yaliyozuia watu wengi kusafiri, alikuwa na uzoefu wa kufanyia kazi mitandaoni.

Katika kipindi hicho anasema mwajiri wake alimuunga mkono.

“Nimekuwa na bodi na wakurugenzi ambao wamenipa ushirikiano kwa asilimia 200 siyo 100 ili kusimamia misingi yetu ambayo ni uwazi, ushiriki na uwajibikaji,” anasema.

Anasema walichukua hatua ya kufungua kesi kudai pasipoti.

“Tulikwenda Mahakama Kuu tukapigwa chini, tukaenda Mahakama ya Rufaa tukasikilizwa, wakafuta uamuzi wa Makama Kuu, ilikuwa Desemba 4, 2020, wakaitaka Serikali irudishe pass (pasipoti) ndani ya siku 60 na siku ya 61 nikapewa,” amesema. 

Baada ya misukosuko, Eyakuze anasema walijadiliana na kuja na mikakati mipya ya kiutendaji iliyopunguza chokochoko kwa Serikali.

“Tukasema tunawezaje kuhakikisha Sauti za wananchi zinasikika bila kuchokoza mkono wa Serikali? Kumbuka tumetoka kwenye sheri ya kampuni tumeletwa kwenye sheria ya NGO,” anasema.

Pia, anasema ni ya Twaweza si kutafuta umaarufu kwa kugombana na Serikali bali kutafuta matokeo ya wananchi.

Eyakuze anayekwenda kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi  ya Ubia wa Serikali ya Uwazi (OGP) aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya uendeshaji ya taasisi hiyo.

OGP ni mpango wa kimataifa unaolenga kupata ahadi kutoka kwa Serikali za kitaifa za kukuza uwazi, kupambana na ufisadi na kuboresha utawala. Unasimamiwa na kamati ya uongozi inayojumuisha wawakilishi kutoka serikalini na mashirika ya kiraia.

Ilianzishwa mwaka 2011, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kwanza alikuwa Sanjay Pradhan. Eyakuze anakuwa wa pili akiwa wa kwanza kutoka Bara la Afrika.

OGP inahusisha nchini 75 na mamlaka 150 za ndani ambazo zinafanya kazi pamoja na maelfu ya mashirika ya kiraia.

Tanzania iliyojiunga na OGP Septemba 2011, New York nchini Marekani chini ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiamo wa Afrika Mashariki, hayati Bernard Membe ilijitoa Julai 2017.

Septemba 20, 2017 aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki alipoulizwa kuhusu sababu ya Tanzania kujiondoa OGP aliahidi kuwa Serikali ingetoa ufafanuzi muda utakapowadia.

Aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Aziz Mlima alikiri Tanzania kujiondoa katika mpango huo.

“Ndiyo ni kweli lakini ni kwa muda tu kwa sababu Serikali inataka kuutathimini mpango huo kama unaendana na masilahi ya Taifa. Kuna mambo tunahitaji kwanza kuyatekeleza kabla ya kutekeleza mpango huu,” anasema

“OGP inailazimu Serikali mwanachama, kila baada ya miaka miwili kutoa taarifa ya mipango na ahadi za mabadiliko yatakayofanywa na kuhakikisha kuna uwajibikaji,” anasema Eyakuze.

Eyakuze pia amewahi kuwa mjumbe wa bodi za Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa kwa Ajili ya Takwimu za Maendeleo Endelevu (GPSDD) na Taasisi ya Ushirikiano kuhusu Uwazi wa Mikataba (OCP).

Related Posts