Janeth Joseph na Florah Temba
Moshi. Mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Azimio, iliyopo Kijiji cha Uchira wilayani Moshi, Dorcas Halifa (13) amejeruhiwa shingoni na kitu chenye ncha kali.
Tukio hilo linaelezwa kutokea alfajiri ya Januari 2, 2025 mtoto huyo alipoagizwa na mama yake mlezi kupeleka maharage mgahawani.
Mtoto huyo aliyeshonwa nyuzi tisa kwenye jeraha inadaiwa alishambuliwa na kijana ambaye alitoweka.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Dickson Mkwazu akizungumza na Mwananchi leo Januari 9, amesema baada ya kujeruhiwa mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, alikoshonwa nyuzi tisa.
Amesema aliyetenda tukio hilo hajafahamika na kwamba mama mlezi wa mtoto huyo alikuwa akihojiwa polisi.
“Polisi walifika nyumbani kwa mama aliyekuwa akiishi na mtoto huyo, walimhoji na kwa sasa suala hilo liko polisi,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 9, 2025 mwanafunzi huyo ambaye amepewa hifadhi kwa msamaria mwema, amesema baada ya kujeruhiwa alirudi nyumbani akapelekwa hospitali.
Amesema baada ya kutoka hospitali walirudi nyumbani ambako mama yake alimfungia ndani kwa kuhofia asidhuriwe tena kisha akaenda kwenye shughuli zake.
Akisimulia alivyojeruhiwa amesema: “Siku ya Alhamisi (Januari 2) niliamka saa 11:00 alfajiri, nikawa naenda hotelini (mgahawani) kwa mama njiani nilikutana na kaka mmoja akaniuliza naitwa nani halafu akawa ameniziba mdomo akanichinja shingo, nilipiga kelele watu hawakusikia, nikarudi nyumbani, mama na baba wakanipeleka hospitali,” amesema.
Amedai mama aliyekuwa akiishi naye alikuwa akimtesa kwa kumpiga.
“Mama alikuwa akiniamsha saa 11:00 alfajiri naenda kudeki kule hotelini halafu narudi kujiandaa kwenda shule,” amesema.
Amedai wakati wa likizo alikuwa akienda kuuza chakula sokoni na anaposahau sahani alikuwa akipigwa.
“Mama alikuwa akinitesa kwa kunipiga mara kwa mara na fimbo ya kusukumia chapati ikitokea nimesahau sahani kwa wateja,” amedai huku akionyesha majeraha aliyonayo mwili.
Mama mzazi wa mtoto huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Salome amesema changamoto za maisha ndizo zilizomfanya amwache mtoto wake kwa mama huyo.
“Nilimwacha mtoto wangu kwa huyu mama nikaenda Arusha kutafuta maisha kutokana na changamoto nilizokuwanazo, lakini kwa kipindi chote nilipokuwa naongea naye kwenye simu hakuwahi kunieleza changamoto alizokuwa anapitia,” amesema.
Ameiomba Serikali kuwachukulia hatua wote waliohusika katika tukio la kujeruhiwa mwanaye.
Jenipha Kasimu, ambaye ni mtetezi wa watoto, amesema walipata taarifa kuhusu kujeruhiwa kwa mtoto huyo Ijumaa Januari 3, 2025 ndipo walipokwenda nyumbani alikokuwa akiishi kumhoji.
Amesema baada ya kumkagua walibaini licha ya jeraha la kukatwa shingoni alikuwa na majeraha mengine mwilini yaliyotokana na kipigo hali iliyowapa wasiwasi, ndipo walipokwenda polisi kuomba uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
“Baada ya kumhoji mtoto tulimkagua mwilini na kubaini kwenye mabega amevimba, lakini pia kwenye mapaja na mwilini alikuwa na majeraha madogo madogo. Tulipomuuliza nini kilitokea alidai alipigwa na mama aliyekuwa akiishi naye,” amesema.
Mmoja wa maofisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto mkoani Kilimanjaro, Mwajabu Mzee amesema matukio ya ukatili kwa watoto yanasikitisha na kwamba wameendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha wanalelewa katika mazingira salama.
“Kutokana na matukio ya ukatili ambayo yameendelea kuripotiwa, niombe wazazi na walezi kuwalea katika malezi na makuzi yaliyo bora, tuepuke kuwaweka mazingira yasiyofaa na kuwatuma kufanya kazi zilizo juu ya uwezo wao, kwani kufanya hivyo ni kutumikisha watoto,” amesema.