Yanga inajiandaa kusafiri kuifuata Al Hilal ya Sudan kwa mchezo wa raundi ya tano ya kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuisaka tiketi ya kupenya kwenda robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu wa pili mfululizo.
Msimu uliopita timu hiyo ilicheza hatua hiyo baada ya kupenya kutoka Kundi A sambamba na Al Ahly ya Misri, lakini ikang’olewa kwa penalti na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo ndani ya dakika 90 iliokolewa na mwamuzi ambaye alikataa bao la Stephane Aziz Ki akidai mpira haukuvuka mstari, kabla ya Rais wa CAF, Patrice Motsepe kusema “kwa maoni yangu lile lilikuwa ni bao halali.”
Yanga imefufua matumaini ya kutinga robo kwa msimu wa pili mfululizo, baada ya wikiendi iliyopita kupata ushindi wa kwanza katika kundi hilo kwa kuifunga TP Mazembe ya DR Congo kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wiki mbili tangu zilipotoka sare ya 1-1 jijini Lubumbashi.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi nne na kutoka mkiani mwa msimamo wa kundi hilo hadi ya tatu, nyuma ya MC Alger ya Algeria yenye pointi tano baada ya Jumapili usiku kutoka sare ya 1-1 ugenini mbele ya vinara, Al Hilal iliyovuna pointi 10 kila timu ikicheza michezo minne.
Kwa sasa Yanga inahitaji kushinda mechi zake mbili zilizobaki na kutinga robo fainali bila ya kujali matokeo ya mechi nyingine.
Jumapili, Yanga itakuwa ugenini dhidi ya Al Hilal, wakati kesho Ijumaa itatangulia mechi kati ya MC Alger na TP Mazembe itakayopigwa huko Algeria.
Mara baada ya mechi hizo za wikiendi hii, Yanga itarudi nyumbani kukabiliana na Mc Alger, wakati Al Hilal itaifuata TP Mazembe inayoburuza mkia kwa sasa kundini ikiwa na pointi mbili baada ya kufumuliwa 3-1 na Yanga Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam.
Wakati hesabu zikiwa hivyo, Yanga ya Sead Ramovic imejitofautisha na ile ya Miguel Gamondi aliyeanza msimu huu wa 2024-25 akiwa na timu hiyo, lakini namba zikimbeba zaidi straika chipukizi, Clement Mzize ambaye alifunga mabao mawili wakati Mazembe ikifa kwa Mkapa.
Mwannanchi linakudadavulia kwa uchache rekodi zinazowatofautisha makocha Ramovic na Gamondi sambamba na namna namba nzima za wachezaji wa Yanga wakiwa chini ya makocha hao katika mechi za Ligi Kuu Bara na zile za Ligi ya Mabingwa Afrika na upepo ulivyo katika timu hiyo ikisaka nafasi ya kwenda robo fainali.
Kocha huyu aliyeinoa timu hiyo tangu msimu uliopita na kuipa mataji ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na Ngao ya Jamii ya msimu huu, mbali na Kombe la Toyota ililotwaa Afrika Kusini, alisitishiwa kibarua Novemba mwaka jana mara baada ya timu huyo kupoteza mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya Azam na Tabora United.
Kabla ya kutimuliwa, kocha huyo raia wa Argentina aliiongoza Yanga katika jumla ya mechi 16 za mashindano, zikiwamo mbili za Ngao ya Jamii ambazo zote timu iliibuka na ushindi, 10 za Ligi Kuu, ikishinda nane na kupoteza mbili na mechi nne za hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa ilizoshinda zote.
Rekodi zinaonyesha kwamba Yanga ya Gamondi ilianza msimu kwa kuifunga Simba kwa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii, kisha ilipotinga fainali ikiifumua Azam FC kwa mabao 4-1.
Baada ya hapo ilifanya kweli katika mechi za awali za Ligi ya Mabingwa kwa kushinda jumla ya mabao 17-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi na CBE ya Ethiopia.
Yanga ya Gamondi ilianza kwa kuichapa Vital’O kwa mabao 4-0 kisha ziliporudiana ikashinda 6-0 na kuifuata CBE kwao na kushinda 1-0 na ziliporudiana jijini Dar es Salaam ikashinda kwa mabao 6-0 na kutinga makundi kwa mara ya pili mfululizo ikiwa chini ya kocha huyo, kwani msimu uliopita pia aliivusha baada ya kupita miaka 25 tangu timu hiyo ilipocheza mwaka 1998 pale Ligi ya Mabingwa ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa.
Baada ya hapo Yanga ikaigeukia Ligi Kuu na kuandika rekodi ya aina yake kwa kucheza mechi nane mfululizo bila kuruhusu bao lolote, huku timu ikishinda mechi zote hizo kabla ya kutenguliwa udhu na Azam katika mechi ya tisa na kufungwa tena mechi ya 10 dhidi ya Tabora United iliyoondoka na kibarua cha Gamondi.
Katika mechi hizo 10, Yanga ya Gamondi ilivuna jumla ya mabao 14 na kufungwa manne, lakini ikitia kibindoni pointi 24, ikiwa haijatoka sare yoyote zaidi ya kupoteza michezo miwili ya mwisho kwa kocha huyo.
Kwa hesabu zote ni kwamba Yanga ya Gamondi kwa msimu huu katika mechi 16 za mashindano yote, ilivuna jumla ya mabao 36 ya kufunga na kufungwa mabao matano tu kabla ya kijiti kumuachia Ramovic ambaye naye ameanza na moto katika Ligi Kuu, huku katika mechi za kimataifa akisuasua tofauti na mtangulizi wake.
Kama ilivyokuwa kwa Gamondi alipoanza msimu huu kwa kasi, ndivyo Ramovic alivyowasha moto katika Ligi Kuu Bara akiwa ameiongoza timu ya Wananchi katika mechi tano na zote imeshinda.
Yanga ya Ramovic haijatoka sare kama ilivyokuwa kwa ile ya Gamondi, pia haijapoteza mchezo wowote hadi sasa, na imeweka heshima kwa kufunga mabao mengi zaidi tofauti na Yanga iliyopita ya Muargentina, kwani imevuna mabao 18 na kuruhusu wavu wa timu hiyo kuguswa mara mbili tu.
Bahati mbaya katika mechi za CAF, Yanga ya Ramovic ilianza na mguu mbaya kwani wachezaji walikuwa wapo chini kimorali kutokana na vipigo viwili vya Ligi vilivyomfuta kazi Gamondi na kuanza mechi za makundi kwa vipigio viwili mfululizo, ikiwa ni rekodi mbaya kwa klabu tangu ianze kushiriki michuano ya CAF.
Yanga ya Ramovic ilianza kwa kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Al Hilal ikicheza Kwa Mkapa, kabla ya kwenda ugenini na kupasuka kwa idadi kama hiyo mbele ya MC Alger ya Algeria, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kupoteza mechi mbili mfululizo za hatua ya makundi tangu 1998.
Hata hivyo, katika mechi ya tatu dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo ililazimisha sare ya 1-1 ikiwa ugenini kabla ya kushinda nyumbani kwa mabao 3-1 ziliporudiana wiki iliyopita na kumfanya katika mechi nne za CAF kama alizozicheza Gamondi wakati akiinoa Yanga msimu huu, Ramovic amevuna mabao manne na kufungwa sita.
Kwa ujumla Ramovic katika mechi tisa alizoiongoza Yanga katika mashindano yote, amevuna jumla ya mabao 22 ya kufunga na kufungwa manane, akiachwa mbali na Gamondi kwa mabao hayo ya kufunga na kufungwa vile vile, japo kila mmoja amepoteza mechi mbili za mashindano yote.
Chini ya Ramovic Yanga imevuna pointi 15 katika Ligi Kuu Bara na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akiwa bado ana mechi mbili za kumalizia hatua ya makundi na nyingine 15 za Ligi Kuu kuona kama atafikia rekodi alizoziacha Gamondi kabla ya kutemeshwa kibarua hivi karibuni.
Ukiachana namba za makocha hao, kwa upande wa wachezaji wote wa Yanga walioliamsha msimu huu chini ya Gamondi na Ramovic, aliyewakimbiza wenzake ni Clement Mzize.
Mshambuliaji huyo chipukizi ameongoza orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi katika mechi zote 25 za mashindano za msimu huu, zikiwamo 16 chini ya Gamondi na tisa za Ramovic, akiwaacha kwa mbali Prince Dube, Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI, Clatous Chama na wengine waliotupia chini ya makocha hao.
Namba zinaonyesha kuwa, katika mechi zote 25, Mzize amefunga jumla ya mabao 12, likiwamo bao moja la Ngao ya Jamii na sita ya Ligi Kuu Bara, huku pia akiwa na mabao matatu ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika na mabao mengine mawili ya hatua ya makundi yote akiitungua Mazembe wikiendi iliyopita.
Mabao hayo 12 ni mbali na asisti alizotoa katika mechi hizo ambazo zimemfanya awe mchezaji aliyehusika na mabao mengi mbele ya Aziz Ki.
Mchezaji anayefuata kwa kufunga mabao mengi katika mechi 25 za Yanga chini ya makocha hao wawili ni Prince Dube ambaye hakuanza vyema katika Ligi Kuu Bara kabla ya kujipata hivi.
Nyota huyo wa zamani wa Highlanders ya Zimbabwe na Azam FC, ndiye anayeshika nafasi ya pili akifunga mabao 10, akitofautiana mawili tu na Mzize.
Dube katika Ligi Kuu Bara amefunga mabao matano yote akiyafunga chini ya Ramovic, lakini ana mabao matatu pia ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika mbali na bao moja la hatua ya makundi ya michuano hiyo na jingine la Ngao ya Jamii wakati Yanga ikiifumua Azam kwa mabao 4-1 Agosti mwaka jana.
Baada ya Mzize na Dube, mchezaji mwingine mwenye mabao mengi katika mechi 25 za Yanga ikicheza chini ya makocha Gamondi na Ramovic, ni Stephane Aziz KI, kwani kiungo mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso amefunga mabao tisa, yakiwa matano ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Aziz KI pia amefunga bao moja katika Ngao ya Jamii, jingine moja la hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mengine mawili ya Ligi Kuu, ambapo pia ameasisti mara nne.
Kama ilivyokuwa kwa Dube, Aziz KI aliyemaliza kama kinara wa mabao wa klabu hiyo na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita alipofunga 21 na kumshinda Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam, hakuanza msimu na kasi, japo kadri siku zikinavyosonga amekuwa akionekana kurejesha makali hasa eneo la kutengeneza nafasi.
Katika mechi iliyopita dhidi ya Mazembe alifunga bao lake la kwanza katika makundi, akiboresha rekodi yake kwani sasa imemfanya awe na jumla ya mabao sita katika michuano ya CAF kwa msimu huu.
Kiungo mshambuliaji huyo aliyemaliza msimu uliopita akiwa kinara wa mabao wa Yanga katika michuano ya CAF wakati timu hiyo ikitolewa robo fainali chini ya Gamondi, akifunga matatu na asisti moja, naye wamo katika orodha ya wakali wa mabao kwa msimu huu chini ya makocha hao wawili.
Pacome amefunga jumla ya mabao matano yote yakiwa ni ya Ligi Kuu Bara, mbali na asisti zake tano za ligi hiyo hadi sasa, akiwatangulia Chama, Maxi Nzengeli na beki Ibrahim Bacca ambao kila mmoja amefunga mabao manne wakicheza chini ya Gamondi na Ramovic.
Maxi amefunga mabao matatu ya Ligi Kuu na moja ya Ngao ya Jamii wakati wakiizamisha Simba kwa bao 1-0, wakati Chama alifunga mabao matatu ya Ligi ya Mabingwa hatua ya awali na jingine moja la Ligi Kuu Bara, wakati Bacca amefunga mabao yote manne katika Ligi Kuu akiwa mchezaji wa nne mwenye mabao mengi katika Ligi kwa mastaa wa Yanga akiwa nyuma ya Mzize, Pacome na Dube.
Wengine waliofunga mabao chini ya makocha hao ni Mudathir Yahya aliyefunga mabao mawili ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa na moja la Ligi Kuu akiwa na jumla ya matatu, huku Mzambia Kenneth Musonda akifuatia nyuma yake akiwa na mabao mawili yote yakiwa ni ya Ligi Kuu Bara, huku Chadrack Boka, Dube Abuya na Jean Baleke wakifunga hesabu kwa kila mmoja kufunga bao moja chini ya makocha hao, huku mabao mengine mawili yakiwa ni ya kujifunga kwa wapinzani.