Polisi mwendo mdundo | Mwanaspoti

NYOTA wa timu ya kikapu  ya Polisi, Lawi Mwambasi amesema ushindi walioupata dhidi ya Yellow Jacket wa pointi 81-70 katika Ligi Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam, ulitokana na kujituma muda wote wa mchezo. 

Mchezo huo uliokuwa mzuri na wa kusisimua ulifanyika kwenye Uwanja wa Bandari, Kurasini na Mwambasi aliiambia Mwanaspoti, licha ya Yellow Jacket kukamia mchezo huo, ila walishindwa kutoboa mbele yake kutokana na namna walivyojipanga mapema.

Polisi iliongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 20-13, robo ya pili Yellow Jacket ilikuja juu ikifunga pointi 28-20.

Hadi kufikia mapumziko, Yellow Jacket ilikuwa inaongoza kwa pointi 41-40, robo ya tatu Polisi iliongoza tena kwa pointi 21-14, kisha 20-15.

Katika mchezo huo Lawi Mwambasi wa timu ya Polisi, aliongoza kwa kufunga pointi 29, aliongoza pia kwa kudaka  mipira ya ‘rebound’ mara nane.

Akifuatiwa na Fahimu Hamad aliyefunga pointi 20, alidaka mipira ya “rebound” mara 7.

Kwa upande wa timu ya Yellow Jacket alikuwa George Mwakyanjala aliyefunga pointi 26 akifuatiwa na Singa Mwitega aliyefunga pointi 18 katika mechi hiyo.

Related Posts