Sababu kuwepo matumaini ya nafuu bei ya mafuta 2025

Miongoni mwa bidhaa muhimu ambazo Tanzania huziagiza nje ya nchi ni bidhaa za mafuta, ambazo gharama zake kwa mwaka ni wastani wa Dola za Marekani 2.57 bilioni (Sh6.1 trilioni).

Kutokana na umuhimu wake katika uchumi, kushuka na kupanda kwa bei za bidhaa hiyo huwa na athari ya moja kwa moja katika maisha ya kila siku ya wananchi na shughuli za kuzalisha mali.

Mwaka uliopita (2024) ulikuwa mgumu kwa upande wa bei za mafuta, ulirithi mwenendo huo mbaya ulioanza mwisho mwa mwaka 2022, lakini mwaka huu (2025) kuna matumaini ya hali tofauti, kwa kuwa sababu zilizochangia hali hiyo zinaelekea kupata ufumbuzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha wauzaji wa mafuta (Taomac), Raphael Mgaya anasema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, zimetokea changamoto kubwa mbili, ambazo hadhani kuwa zinaweza kujitokeza tena mwaka huu.

“Mwaka uliopita tumepitia changamoto ngumu ambayo waagizaji hatukuwahi kuipata tangu tuwe chini ya udhibiti wa Serikali, nayo ni uhaba wa dola za Marekani, pia kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita tumekuwa katikati ya changamoto za vita vya mataifa muhimu katika usambazaji wa mafuta,” anasema.

Anasema vita kati ya Russia na Ukraine pamoja na vile vya Gaza vimekuwa na athari kubwa katika uzalishaji na usambazaji wa mafuta, jambo ambalo liliathiri bei ya bidhaa hiyo muhimu katika uchumi.

“Maeneo hayo yenye vita ni maeneo ya kimkakati katika biashara ya mafuta duniani na mnyororo wake wa thamani, sasa hali ya mafuta duniani inaanza kuimarika, hatutarajii makubwa zaidi ya hayo yaliyotokea, hivyo huenda mambo yakazidi kuwa mazuri,” anasema.

Kuhusu mabadiliko ya utegemezi wa nishati duniani nayo kuwa na mchango wa kuwa na utulivu wa mafuta, Mgaya anasema hilo athari zake zinaweza kuonekana baada ya muda mrefu si kwa kipindi kifupi au cha kati.

Kuhusu mwenendo wa bei ya mafuta nchini Kamishna wa. Petroli na Gesi, Wizara ya Nishati Goodluck Shirima anasema kama mambo hayatabadilika kuna matumaini ya unafuu wa nishati hiyo.

“Tusipoathiri na mambo yaliyo nje ya mipaka yetu kwa sera tulizonazo tunaamini kuwa mafuta yataendelea kupatikana kwa bei himilivu kwa wananchi,” anasema na kuongeza kuwa sera ya uagizaji wa mafuta kwa pamoja ina ufanisi mzuri.

Matumaini ya kuwa na bei nzuri ya mafuta pia inatokana na kuimarika kwa Shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu za kigeni, jambo ambalo limepunguza gharama za uagizaji wa bidhaa za nje, pindi viwango vya kubadilishia fedha za kigeni vinapoongezeka na gharama za bidhaa zitokazo nje nazo huongezeka.

Mwanzoni mwa Oktoba, 2024 viwango vya kubadilisha Dola moja ya Marekani vilifikia karibu Sh2,800, lakini mpaka jana viwango vya kubadilisha sarafu hiyo vilikuwa kwa wastani wa Sh2,401.34 kwa mujibu wa Benki Kuu (BoT).

Kutokana na kuimarika kwa Shilingi, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alilieleza gazeti la The Citizen, kuwa hali ya kuimarika kwa Shilingi inatarajiwa kuendelea hadi Februari 2025.

Alieleza kuwa matarajio hayo yanatokana ongezeko la uzalishaji wa mazao muhimu kama korosho inayouzwa sasa pamoja na mahindi na mpunga baadaye mwezi huu.

“Mpango wa kufadhili usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi (Export Guarantee Scheme) uliozinduliwa Juni 2023, umeongeza thamani na wingi wa mauzo ya mazao nje ya nchi,” alisema Tutuba. Pia alibainisha kuwa miradi ya Stamico inatarajiwa kupewa dhamana ili kuchochea uzalishaji zaidi.

Aliendelea kuwa Tanzania sasa inazalisha bidhaa za kioo, vigae na nyaya za umeme, jambo ambalo limepunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje. Aidha, bei ya mazao kama kahawa na korosho imeongezeka kutokana na mipango kama Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Sekta ya utalii nayo imeonyesha ukuaji, licha ya kuingia msimu wa utulivu. Tutuba aliongeza kuwa juhudi za kuhimiza matumizi ya Shilingi badala ya sarafu za kigeni zimepunguza mahitaji ya Dola za Marekani.

Kuhusu hali ya uchumi wa dunia, alisema kushuka kwa thamani ya Dola ya Marekani kumesababishwa na sababu za kimataifa, ikiwa ni pamoja na ongezeko la uzalishaji baada ya janga la Uviko-19.

Hali ya bei ya mafuta sasa

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kwenye mtandao wa Trading Economics (TE), bei ya pipa moja la mafuta ghafi iliongezeka kwa Dola 2.22 tangu Januari mosi hadi jana Januari 8, 2025 lilipouzwa Dola 76.96, sawa na ongezeko la asilimia 2.79.

Uchambuzi wa mtandao wa TE unaonyesha kuwa pipa moja linatarajiwa kuuzwa kwa Dola 76.23 ifikapo mwisho wa robo ya kwanza ya mwaka huu na kufikia Dola 81.21 mwishoni mwa mwaka huu. Kiwango hicho kinaelezwa na wachambuzi kuwa si kibaya sana.

Bei kubwa ya mafuta kwa pipa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ilikuwa ni Dola 120 kwa pipa, Juni 2022 na kiwango cha chini zaidi ni Dola 21, Aprili 2020 wakati ambao mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 ulikuwa umeshika hatamu.

Bei iliyopo sasa inatajwa kuchangiwa na hofu juu ya upatikanaji mdogo wa mafuta ya Urusi na Iran kutokana na kuongezeka kwa vikwazo vya Magharibi wanavyokabiliana navyo na huenda bei ingekuwa ndogo zaidi kama hali ingekuwa tofauti.

Pia kuna hofu juu ya upungufu wa usambazaji umeongeza mahitaji ya mafuta ya Mashariki ya Kati, kama inavyoonekana katika uamuzi wa Saudi Arabia kuongeza bei ya mafuta kwa mataifa ya Asia ifikapo Februari.

Kadhalika nchini China, hatua ya bandari ya Shandong kupiga marufuku meli za mafuta zilizowekewa vikwazo na Marekani kufika bandarini mwake inaweza kuzuia ufikiaji wa vituo muhimu.

Zaidi ya hayo, hali ya hewa ya baridi kali nchini Marekani na Ulaya imeongeza mahitaji ya mafuta ya kupasha joto, na hivyo kuchangia ongezeko la bei.

Hata hivyo, kuna matumaini kuwa Rais Mteule wa Marekani anaweza kumaliza migogoro ya kikanda, hivyo kuweka utulivu wa kiuchumi na amani ulimwenguni. Trump anatarajia kuapishwa Januari 20, 2025.

Baada ya kuchaguliwa kwake ulimwengu ulipata matumaini kuwa huenda sasa migogoro inayoendelea ikifikia ukomo. Kwa ujumla migogoro inayoendelea pamoja na sera za Marekani juu ya nishati na udhibiti wa mfuko wa bei vimeathiri bei ya mafuta ulimwenguni.

Kuhusu hoja ya Trump kuleta nafuu ya nishati ya mafuta kutokana na sera zake alizojitanabahisha nazo, Mwenyekiti wa Umoja wa watoa huduma za mafuta na gesi nchini (ATOGS), Abdusamad Abdulrahim anasema hana imani na hilo kutokana na uzoefu wa uongozi wa Trump katika mhula wake wa kwanza.

“Vipaumbele vya Trump ni kufanya kazi na wabia wa Marekani tena wanaokubali kutumia Dola (sarafu ya Marekani), lakini pia kuendeleza ukubwa wake ulimwenguni. Washirika wa karibu wataneemeka, lakini wale wa chini wanawekwa kando,” anasema Abdulrahim.

Anasema nafuu kidogo inayoonekana sasa ni matumaini waliyobeba watu baada ya kuchaguliwa kwa Trump, lakini akiwa kama alivyokuwa katika muhula wake wa kwanza huenda hali ikawa tofauti. “Ni mapema mno kuwa na imani ya hali ya mambo binafsi, naamini tujipe muda,” anasema Abdulrahim.

Related Posts