Serikali yaahidi upatikanaji maji maeneo matano Dar

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew amesema maeneo yaliyokuwa na changamoto ya huduma ya majisafi ya Kinyerezi, Ukonga, Kitunda, Kibamba na Mwanagati jijini Dar es Salaam yanakwenda kupata huduma ya kutosheleza.

Hatua hiyo inatokana na mradi wa Bangulo unaogharimu kiasi Sh36.8 bilioni ukitarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 450,000 ukijumuisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lita milioni tisa na ulazaji wa mtandao wa bomba wenye kilomita 108 kukamilika Januari 30, 2025.

Leo Alhamisi, Januari 9, 2025, Kundo ametembelea mradi wa maji Dar es Salaam ya Kusini unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kujionea maendeleo yake.

“Niseme sasa muarobaini wa huduma ya majisafi umepatikana katika maeneo ya Kinyerezi, Ukonga, Kitunda, Kibamba na Mwanagati maeneo haya yaliyokuwa na changamoto ya majisafi sasa yanakwenda kupata huduma ya kutosheleza,” amesema Kundo.

Kundo amesema kazi kubwa inafanyika chini ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani pamoja na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Kwa upande wake, Ayubu Mwaikotobwa ambaye ni Mwakilishi Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa, ameeleza fedha hizo za utekelezaji wa mradi wa maji Bangulo ni ishara kubwa ya upendo wa Rais kwa wananchi wa Ukonga na meneo jirani yatakayonufaika na mradi na  sasa wananchi wa maeneo hayo wanaimani kubwa ya kupata huduma ya majisafi na salama ya kutosheleza.

Katika hatua nyingine, jana Jumatano, Januari 8, 2025 Kundo alitembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu na kuridhishwa na utekelezaji wake unaonufaisha zaidi ya wakazi 200,000 wa Mji wa Chalinze.

Akizungumzia na wakazi wa Kata ya Msata alipotembelea moja ya vizimba vinavyohudumia wakazi wa eneo hilo, Kundo aliipongeza Dawasa kwa kazi nzuri ya usimamizi wa mradi na kuagiza kazi chache zilizosalia zikamilishwe kwa wakati.

“Nichukue nafasi hii kuwaagiza Dawasa, kuna baadhi ya vizimba vilivyojengwa wakati wa awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huu na sasa havitoi maji, mkavirekebishe na wananchi wapate huduma, lakini pia katika awamu hii ya tatu ya mradi mkandarasi ahakikishe vizimba vyote vinatoa maji kabla ya kukabidhi mradi huu,” amesema Mhandisi Kundo.

Kundo amesema kwakuwaomba wananchi kuilinda miundombinu ya maji kwa wivu mkubwa ili thamani ya fedha iliyotumika iendelee kuonekana.

“Sisi Wizara ya maji hatutakaa ofisini, tutatoka kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa ipasavyo na wananchi wanapata huduma ili adhima ya Rais ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani iweze kukamilika,” amesema Kundo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga amemshukuru naibu waziri kwa ziara yake kwani imekuwa ya mafanikio na wanabaki na imani kubwa huduma ya maji katika maeneo ya Bagamoyo na Chalinze itaimarika zaidi.

Related Posts