Tanzania na Japan zimetia saini hati ya Makubaliano (MoU) ya utekelezaji miradi ya huduma za Afya lengo likiwa kuboresha huduma hizo na kuhuisha ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa kuzingatia vipaumbele vya pamoja.
Utiaji Saini wa makubaliano hayo umefanyika mapema leo tarehe 8 Januari, 2025 katika ukumbi wa Wizara ya Afya kati Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama na Balozi wa Japan anayemaliza muda wake Mhe. Yasushi Migawa.
Akiongea mara baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameyataja maeneo ya ushirikiano kuwa ni uboreshaji wa huduma nje ya vituo, rufaa na huduma za kibingwa katika ngazi zote za utoaji huduma za Afya.
Mengine ni kusaidia kuanzisha utekelezaji wa mifumo ya Bima ya Afya kwa wote ili kupunguza ukosefu wa usawa katika hutoaji huduma za afya pamoja na huduma za uchunguzi, kinga,tiba, huduma za utengamao na tiba shufaa katika ngazi zote za huduma.
Aidha Waziri Mhagama ameyataja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa ni kuboresha huduma za uzazi, afya ya mama na mtoto, kuzia na kudhibiti magonjwa ya milipuko na matukio mengine ya dharura za Afya.
Waziri Mhagama ameongeza kuwa maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na kuboresha utekelezaji wa huduma za matibabu kwa njia ya masafa na mifumo ya taarifa za afya katika ngazi zote za huduma, kusaidia utekelezaji wa tiba asili na tiba mbadala nchini Tanzania ikiwemo pia kubadilishana uzoefu na ujuzi katika usimamizi wa hospitali.
Mhe Mhagama amesema Tanzania ipo mbioni kujenga kituo cha umahiri cha usambazaji wa teknoliojia ya tiba ya figo hapa nchini pamoja na nchi jirani, suala ambalo litaijengea Tanzania heshima kubwa katika anga za kimataifa.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Yasushi Migawa amesema Serikali ya Japan inaweka vipaumbele katika usalama wa binadamu ndio maana itaendelea kuwekeza katika huduma za afya kwa nchi za Afrika kama ambavyo imekuwa ikifanya katika nchi za Asia.
Balozi huyo ameongeza kuwa pamoja na kwamba anamaliza muda wake hapa nchini ni imani yake kuwa mrithi wake katika nafasi hiyo ataendeleza yale mazuri ambayo Serikali yake imeendelea kuyatekeleza katika suala zima la sekta ya afya.
Aidha Balozi Migawa ameongeza kuwa Serikali yake imekuwa ikitekeleza miradi ya afya kupitia mashirika makubwa ya nchini Japan, akibainisha kuwa miradi hiyo imekuwa ikitekelezwa kupitia shirika la JAICA na mashirika mengine yanayojitolea kutoa elimu ya juu ya fani ya udakitari nchini mwake.
Balozi Migawa ameyataja maeneo mengine muhimu ambayo Serikali yake imekuwa ikitekeleza kwa upande wa afya ni pamoja na kusaidia huduma za upandikizaji wa figo hospitali ya Benjamini Mkapa ikiwemo ufadhili wa masomo nchini Japan.