Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Naibu Waziri, Cosato Chumi aliongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa mashauriano na ujumbe wa Norway ikiwa ni matokeo ya Hati ya Makubaliano iliyosainiwa baina ya nchi hizo mwaka 2017 kwa lengo la kuanzisha mikutano ya mashauriano ya kisiasa kila mwaka kupitia mwenendo wa ushirikiano na kubainisha maeneo mapya ama yenye kuhitaji nguvu zaidi katika ushirikiano.
Akizungumza wakati wa mashauriano hayo Naibu Waziri Chumi ametaja maeneo ya ushirikiano kati ya Tanzania na Norway katika sekta za maendeleo, biashara, nishati, afya, elimu, mabadiliko ya tabia nchi na kilimo. Bila kusahau misimamo ya pamoja katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, kulinda amani na usalama duniani, na kulinda haki za binadamu.
Mhe. Chumi amezitaja pia fursa zilizopo ambazo kwa pamoja zinaweza kuangaliwa vyema na kutendewa kazi, likiwemo eneo la biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili. Huku biashara ya Tanzania ikiongezeka, wigo wa uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Norway bado ipo chini, hususan katika sekta ya miundombinu, nishati, kilimo na usindikaji. Kubadilishana maarifa na teknolojia ni eneo lingine la kunufaika nalo.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Norway, Mhe. Andreas Kravik anasema Norway inajivunia kuhusishwa na Tanzania na ipo tayari kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kutoa wito wa ushirikiano kati yake na Serikali pamoja na sekta na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Pia alitoa wito wa ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kupambana na milipuko na umaskini, akisisitiza ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia.
Aidha, Mhe. Kravik ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ziara yake nchini Norway mwaka jana na kupongeza zaidi juhudi za Tanzania katika kupambana kikamilifu na mabadiliko yatabianchi duniani na kuwa kinara wa mpango wa Nishati Safi ya Kupikia.