Dar es Salaam. Wakati huduma ya usafiri wa treni ya kisasa ya umeme (SGR) ikirejea alfajiri ya kuamkia leo Alhamisi, Januari 9, 2025, uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) umesema kilichosababisha hitilafu ya usafiri huo si ubovu wa treni iliyokuwa imebeba abiria.
Imesema, njia ya treni hiyo ndiyo ilifungwa baada ya behewa moja kutoka kwenye reli na kukanyaga chini wakati wakifanya ‘shunting’, hali iliyosababisha kuzuia treni nyingine kuendelea na safari.
Abiria waliokuwa wakitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma walilazimika kupandishwa mabasi kutoka Ihumwa, baada ya treni hiyo kutoendelea na safari katika eneo hilo.
Inaelezwa, treni hiyo ilipofika Morogoro ilisimama kwa saa kadhaa kabla ya kuendelea na safari na ilipofika Ihumwa abiria walitakiwa kushuka ili kupanda mabasi hadi Dodoma.
Taarifa ya TRC ilisema changamoto hiyo ilisababishwa na hitilafu ya kiufundi kwenye kituo cha Ihumwa.
Ilisema safari za kawaida ziliathirika ikisisitiza mafundi wanarekebisha tatizo kuhakikisha huduma zinarejea kwenye hali ya kawaida.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 9, 2025, Mkurugenzi wa Oparesheni wa TRC, Focus Sahani amesema tayari huduma zimerejea tangu alfajiri ya kuamkia leo.
“Tulifungua njia saa 6 usiku na huduma kuendelea kama kawaida,” amesema Sahani akifafanua hitilafu iliyotokea haikuwa ya treni iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma.
“Njia ilizibwa baada ya moja ya behewa kuacha reli na kukanyaga chini likazuia njia kwa treni nyingine kuendelea na safari,” amesema.
Amesema, behewa hilo walitaka kuliongeza kwenye treni iliyokuwa ikitoka Dodoma usiku wa Januari 7, 2025.
“Treni iliyokanyaga chini ilikuwa inafanya shunting, tulitaka kuongeza behewa jingine kwenye treni ya usiku ya kutoka Dodoma pale Ihumwa,” amesema.
Akifafanua sababu ya behewa hilo kuacha reli na kukanyaga chini, Sahani amesema ni hitilafu za kiufundi kwa kuwa behewa hilo lilikanyaga eneo la maungio.
“Huenda kulikuwa na shida kwenye maungio, hivyo ni hitalafu tu, changamoto hii ilichukua muda kidogo hadi kuitatua kwa kuwa ilipaswa inyanyuliwe na kutolewa kwenye njia, zoezi ambalo lilichukua muda na kuzuia treni nyingine kupita,” amesema.
Amesema, changamoto hiyo ilirekebishwa na kukamilika usiku wa jana na alfajiri ya kuamkia leo huduma ya treni iliendelea kama kawaida.
Usiku wa jana Jumatano, TRC kupitia kwa Kitengo cha Habari na Uhusiano kilitoa taarifa kwa umma ikizungumzia tatizo hilo lililosababisha mabadiliko ya ratiba huku ikiwaomba radhi abiria kutokana na usumbufu walioupata.
“Shirika la Reli Tanzania (TRC), linapenda kutoa pole kwa abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma Januari 8, 2025 kufuatia usumbufu uliojitokeza kutokana na hitilafu ya kiufundi iliyotokea katika kituo cha Ihumwa Dodoma saa 5:38 usiku.”
“Tunajua kuwa safari zetu za kawaida kati ya Dar es Salaam na Dodoma zimeathirika na tunatambua kuwa hii inaweza kuwa na athari kubwa kwenu. Shirika linaendelea kuomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza,” ilieleza taarifa hiyo.