Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, amezuwa mjadala mkali kimataifa baada ya kutaja uwezekano wa kuuchukuwa Mfereji wa Panama, kisiwa cha Greenland na kuigeuza Canada kuwa jimbo la 51 la Marekani.
Kauli ya Trump imekemewa vikali na viongozi wa nchi za magharibi pamoja na Canada. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Fllorida hapo jana, alisema hawezi kuondosha uwezekano wa kutumia nguvu za kiuchumi au kijeshi kutwaa udhibiti wa Mfereji wa Panama na Greenland.
Kwa upande mwengine, Trump alikosowa vikali utumiaji wa bidhaa za Canada na pia msaada wa kijeshi wa Marekani kwa jirani yake huyo, akidai mpaka baina yao ni wa kubuni.
Kuhusu Greenland, kisiwa chenye utajiri wa rasilimali kinachomilikiwa na Denmark, Trump alisema atatumia shinikizo la kiuchumi ikiwa Copenhagen itakataa kuiuzia Marekani kisiwa hicho.
Waziri Mkuu wa Canada, Justin Treudau, amemkosowa vikali Trump kwa kauli yake hiyo, huku Panama ikisema hakuna namna yoyote ambapo itayatowa mamlaka yake kwa Marekani.
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, amesema asahau; kisiwa cha Greenland hakiko kwenye mnada.