Vikosi vya SMZ vyaanzisha miradi kujiongezea mapato

Unguja. Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali amesema ujenzi wa miradi unaofaywa na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) utawezesha mapato kupatikana na kutatua mahitaji ya msingi bila kusubiri mgawanyo wa fedha za bajeti.

Amesema fedha za bajeti zinasubiriwa na wengi na haziwezi kumaliza mipango ya vikosi hivyo, kwani hupatikana kwa uchache na kwa kuchelewa.

Amesema hayo wakati wa uwekaji jiwe la msingi la kituo cha kuuzia mafuta makao makuu ya Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) leo Januari 9, 2025.

“Majukumu yenu ni makubwa kama kikosi na mengine ni ya haraka, hivyo kusubiri fedha za bajeti ya Serikali ili muweze kuyatimiza ni kujichelewesha,” amesema.

Amesema kuna majukumu ambayo wanapanga kwenye bajeti lakini mengine yanatokea nje ya mipango na bajeti, ambayo yanahitaji kutekelezwa kwa uharaka bila ya kusubiri bajeti ya Serikali, hivyo miradi ya aina hiyo itawaweka mahali pazuri pa kutekeleza majukumu hayo.

Ameeleza ujenzi wa miradi ya uzalishajimali ni utekelezaji mzuri wa maagizo ya Raisi wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika kuwajengea mazingira bora ya kufanyia kazi maofisa na wapiganaji wa idara maalumu ya SMZ, ikiwemo KVZ.

Hata hivyo, amemtaka Kamanda Mkuu wa KVZ, Said Juma Shamuhuna kuweka utaratibu mzuri wa matumizi wa kituo hicho cha mafuta na majengo mengine yaliyokuwepo ili yaendelee kutumika kwa muda mrefu.

“Ni matumaini yangu kuwa kituo hicho kitakapomalizika kitakuwa ni cha aina yake kwa upande wa majengo, ubora, uzuri wake pamoja na huduma zake. Tunatarajia wahudumu na walinzi wa hapa watakuwa watu wenye sifa nzuri na watakaoipatia KVZ sifa ya utoaji wa huduma nzuri,” amesema.

Akitoa taarifa za kitaalamu, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu (TMSMIM), Issa Mahfoudh Haji amesema ujenzi wa kituo hicho ni hatua ya kutatua changamoto ya ukosefu wa miradi unaorudisha nyuma utendaji kazi.

Amesema mradi huo umegharimu Sh1 bilioni na utakapokamilika utasaidia upatikanaji wa mafuta kwa kikosi na kuimarisha ulinzi katika maeneo yao kwa wakati husika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia viongozi wakuu wa kitaifa, Machano Othman Said amesema kikosi kinaendelea kufanya vizuri katika ujenzi wa miradi. Amesema kamati inaridhishwa na utendaji kazi wake.

Amesema awali hawakuwa katika utendaji mzuri, hivyo baada ya kuliona hilo kikosi kilipewa ridhaa ya kufanya shughuli za kibiashara.

Related Posts