Waliofaulu darasa la nne, kidato cha pili waongezeka wadau wakionya

Dar es Salaam. Wakati idadi ya wanafunzi waliopata daraja A hadi C katika mtihani wa upimaji darasa la nne na daraja la I hadi la III katika mtihani wa upimaji kidato cha pili ikiongezeka, wadau wa elimu wametoa wito wa kufanyika tathimini ya kujua ni wanafunzi wangapi wanatoka katika shule za Serikali.

Wadau waliozungumza na Mwananchi leo Januari 8,2025, wamebainisha kuwa mchanganyiko wa matokeo ya shule za Serikali na binafsi unaweza kutoa taswira isiyo sahihi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa, hasa kwa upande wa shule za Serikali ambazo wanafunzi wengi hukumbana na changamoto ya lugha ya Kiingereza.

Kauli hizo zimetolewa kufuatia uchambuzi wa matokeo ya mitihani ya upimaji yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Januari 4, 2025.

Matokeo hayo yanaonesha ongezeko la wanafunzi waliopata daraja A hadi C kwa darasa la nne kutoka 809,379 mwaka 2023 hadi kufikia 931,468 mwaka 2024.

Kwa mwaka 2023, wanafunzi waliopata ufaulu huo walikuwa sawa na asilimia 52.38 ya wanafunzi wote walioketi kufanya mtihani huo wa upimaji, huku kwa kidato cha pili, asilimia ya watahiniwa waliopata ufaulu huo ikiwa 60.85.

Matokeo hayo yalisababisha wastani wa shule zilizopata daraja A hadi C kupanda kwa asilimia 10 kutoka asilimia 54.20 mwaka 2023 hadi asilimia 64.20 mwaka 2024.

Hii inamaanisha kati ya shule zote 20,036 zilizoshiriki mtihani wa upimaji darasa la nne, shule 12,865 zilipata wastani wa daraja A hadi C.

Hata hivyo, ufaulu huu unaongeza changamoto nyingine, idadi ya wanafunzi walioketi kwa ajili ya mtihani wa majaribio darasa la nne ilipungua kutoka 1,545,330 mwaka 2023 hadi wanafunzi 1,530,805 mwaka 2024.

Hali hii pia ilionekana kwa wanafunzi wa kidato cha pili, ambapo idadi ya waliopata daraja la I hadi III iliongezeka kutoka 192,633 mwaka 2023 hadi kufikia 239,707 mwaka 2024.

Ongezeko hili lilisababisha pia idadi ya shule katika makundi ya umahiri kuongezeka. Kati ya shule 5,900 zenye matokeo, shule 1,570 sawa na asilimia 26.61 zilipata wastani wa Daraja A hadi C, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.46 ikilinganishwa na mwaka 2023.

Kukua kwa ufaulu huu huenda kumechangiwa na ongezeko la wanafunzi wa kidato cha pili walioketi kwa ajili ya mtihani wa upimaji, sababu mwaka 2024 watahiniwa walikuwa 796,825 kutoka 694,769 wa mwaka 2023.

Mdau wa elimu, Catherine Sekwao akizungumzia hilo amesema kuna haja ya kufanya mlinganisho kati ya shule za binafsi na za Serikali.

Amesema baadhi ya shule binafsi hazina daraja la pili hadi sifuri, huku shule za Serikali zikiwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliopata daraja la nne na sifuri.

“Tutenganishe tuone kuna nini hakifanyiki, siku hizi hali imebadilika ni kama inamarika, lakini tukichukua shule za Serikali peke yake, matokeo yasingekuwa mazuri sana. Tunahitaji kujitahidi zaidi kwa sababu wanaofeli bado ni wengi,” amesema Sekwao.

Amesema haoni sababu ya kutofanyika kwa mlinganisho kati ya shule za Serikali na binafsi ili kubaini changamoto zilizopo, huku akisisitiza kuwa tatizo kubwa linaloonekana ni lugha kwa shule hizo.

Mkurugenzi wa Tanzania Education Supporting Agency (Tesa), Mussa Badi amesema ongezeko la ufaulu linaloonekana huenda limechangiwa na kuongezeka kwa walimu wanaoajiriwa ambao wanapewa mafunzo na mbinu mbalimbali za ufundishaji.

Amesema hatua hiyo inakwenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia, unaotekelezwa kupitia ujenzi wa shule mpya na uwekaji wa madawati.

“Watoto wanakaa katika madawati, hawakai chini. Hii inawapa uhuru zaidi wa kujifunza. Jambo jingine kubwa ni walimu kuwezeshwa,” amesema.

Aidha, amebainisha kuwa licha ya ufaulu kuongezeka, bado idadi ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ni ndogo.

“Ukilinganisha na wanafunzi waliopata daraja sifuri na la nne, bado kuna idadi kubwa ya waliopo katika madaraja hayo ya chini. Ni muhimu kutafuta mbinu zitakazowasaidia wanafunzi wengi zaidi kufikia daraja la kwanza hadi la tatu,” amesema.

Ameongeza kuwa idadi ya wanafunzi waliopata daraja la nne na sifuri katika mtihani wa kidato cha pili bado ni kubwa. Hii ni ishara kwamba kuna haja ya kuweka mkazo zaidi katika kuwapa wanafunzi ujuzi mbadala, ikiwemo ufundi stadi, ili kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Related Posts