Wanaodaiwa kunaswa na jahazi lenye kilo 447 za dawa za kulevya kortini

Dar es Salaam. Raia wanane wa Pakistani wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kusafirisha jumla ya kilo 447.3 za dawa za kulevya aina ya heroine na ethamphetamine.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo, leo Alhamisi Januari 9, 2025 na kusomewa mashtaka yao, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Washtakiwa hao ni Mohamed Hanif (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pehilwam (50) maarufu kama Tayeb, Immambakshi Kudhabakishi (55).

Wengine ni Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45).

Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashtaka hayo, mmoja wa washtakiwa alidai kuwa hawajui lugha yoyote zaidi ya lugha yao na kwamba Kiingereza hawakijui vizuri, hivyo wanaomba watafutiwe mkalimani atakayetafsiri kutoka Kiingereza kwenda lugha yao ya Kipakistani.

“Hakimu, hawa wenzangu wote wanajua lugha ya Urdu tu, hawajui Kiingereza, hata mimi hapa Kiingereza najua kidogo sana yaani kwa mbali,” alidai mshtakiwa, Hanif ambaye alitumia lugha ya Kiingereza.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilitafuta mkalimani wa lugha hiyo.

Mkalimani huyo, Salma Mohamed, raia wa Pakistani, alifanya tafsiri kutoka Kiingereza kwenda lugha ya Urdu ambayo inatumika nchini Pakistani.

Baada ya kupatikana mkalimani huyo, Wakili wa Serikali Titus Aron aliieleza Mahakama hiyo kuwa washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025.

Wakili Aron, baada ya kueleza hayo, Hakimu Nyaki aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Akiwasomea mashtaka yao, wakili Aron alidai kuwa katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kemikali ya kutengenezea dawa.

Alidai kuwa washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 25, 2024 katika eneo la Navy lililopo Kigamboni, Wilaya ya Kigamboni, ambapo kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 424.77 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine.

Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kuelvya aina heroin, tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 25, 2024 eneo la Navy Kigamboni, ambapo washtakiwa hao walikutwa na heroin zenye uzito wa kilo 22.53.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Nyaki alisema washtakiwa wataendelea kubaki rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 22, 2025 itakapotajwa

Related Posts