Watoto yatima vituo tisa wapatiwa sare, vifaa vya shule

Dar es Salaam. Wazazi na walezi nchini wamekumbushwa kuzingatia suala la kulea watoto katika ngazi ya familia ili wapate huduma za malezi bora na upendo wa dhati kutoka kwa baba na mama pamoja na ndugu wa karibu.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Januari 9, 2025 na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis wakati wa hafla ya kukabidhi sare na vifaa vya shule kwa vituo tisa vya makao ya kulelea watoto yatima Dar es salaam vilivyotolewa na Taasisi ya Lalji Foundation.

“Sio kila mtoto anayelelewa katika vituo hana wazazi bali kuna sababu mbalimbali ambazo zinapelekea kulelewa katika vituo hivyo, lakini endapo watoto wakilelewa katika ngazi ya familia itasaidia kupunguza idadi ya wanaolelewa katika vituo hivi,” amesema.

Aidha, ameipongeza na kuishukuru taasisi hiyo kwa kuiunga mkono Serikali kuboresha mazingira ya sekta ya elimu nchini, huku akitoa wito kwa wadau wengine kujenga utamaduni wa kusaidia watu wenye uhitaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa taasisi hiyo ya Lalji, Imtiaz Lalji amesema lengo lao ni kuendelea kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji na akibainisha msaada huo waliotoa kwa watoto yatima utawawezesha kielimu.

“Tunaelewa upatikanaji wa elimu na rasilimali muhimu kama vifaa vya shule ni nyenzo muhimu sana katika kufungua fursa za watoto kutimiza ndoto zao hivyo basi hiyo ndo sababu kubwa ambayo imetupelekea kusaidia watoto hawa kupata vifaa wanavyohitaji kufikia malengo yao ya elimu,” amesema.

Imtiaz amepongeza juhudi na kazi kubwa inayofanywa na wasimamizi wa vituo vya kulea watoto yatima nchini kwa kujitolea muda na nguvu zao katika kulea watoto hao.

Katibu wa Lalji, Fatema Lalji amesema jumla ya watoto 400 kutoka makao tisa ya kulea watoto yatima Dar es Salaam wamepatiwa msaada huo na kubainisha taasisi inasaidia vituo vya watoto yatima kila mwisho wa mwaka kwa kuwapa sare za shule, mabegi, viatu, soksi kupitia mradi huo endelevu ambao unatekelezwa kila mwaka.

Akizungumza kwa niaba ya walezi wa vituo tisa vya kulelea watoto yatima ambavyo vimepatiwa msaada huo, Mama Mutemwa kutoka kituo cha Bibi na Babu ameishukuru Lalji kwa kutoa msaada huo kwani utasaidia watoto hao kuhudhuria masomo bila changamoto ya vifaa.

“Pia itawasaidia kutimiza ndoto zao na nitoe wito kwa wadau wengine kuendelea kupeleka misaada kwani uhitaji bado ni mkubwa,” amesema Mutemwa.

Related Posts