Yassin Mustafa aibukia Tabora United

BAADA ya kukaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita tangu alipomaliza mkataba na Mtibwa Sugar, beki Yassin Mustapha amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Tabora United.

Mustapha ameenda Tabora kuziba pengo la aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Said Mbatty aliyeachwa na kukimbilia Fountain Gate katika dirisha dogo la usajili lililo wazi na litakalofungwa wiki ijayo.

Akizungumza na Mwanaspoti, beki huyo wa zamani wa Polisi Tanzania na Yanga, alisema baada ya kukaa nje nusu msimu anarudi kupambana upya na ameahidi kuipambania timu hiyo ili iweze kufikia mafanikio waliyojiwekea tangu mwanzo mwa msimu huku akiweka wazi kuwa haitakuwa rahisi kwake lakini yupo tayari kupambana.

“Nilikuwa nje yab uwanja kutokana na kuamua kupumzika kwa muda baada ya kumaliza mkataba wangu na Mtibwa Sugar na lilikuwa nje kwenye mechi za mashindano tu lakini nilikuwa najifua na nipo fiti tayari kwa mapambano,” alisema Mustafa na kuongeza;

“Nimeaminiwa nimepewa mkataba wa mwaka mmoja sasa ni wakati wangu kuonyesha ni kwanini nimeipata nafasi hii, nitapambana kwa kusaidiana na wenzangu ili kuisogeza timu hii hatua moja hadi nyingine, hili linawezekana.”

Alisema anawaheshimu wachezaji wote waliopo ndani ya kikosi hicho, hamuhofii mtu kwasababu anaamini katika kipaji na uwezo alionao ikiwa ni pamoja na uzoefu alionao katika Ligi Kuu.

Beki huyo wa kushoto ambaye maisha yake ya soka alianzia Dodoma katika timu ya Shelly pia amewahi kuzichezea timu za Polisi Dodoma, Stand United, Mwadui United, Coastal Union na Polisi Tanzania.

Related Posts