RAFIKI yetu Nasreddine Nabi wakati anakuja nchini kwa mara ya kwanza kufanya kazi ya kuinoa Yanga, hakukuwa na mbwembwe wala hekaheka nyingi za vyombo vya habari.
Ilikuwa hivyo kwa sababu hakuingia kama staa kwa vile alitoka kuachana na El Merreikh ya Sudan kufuatia mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na ligi kuu kule Sudan.
Hivyo ni kama watu walikuwa na wasiwasi naye kuanzia mashabiki, viongozi wa Yanga hadi waandishi wa habari ambao waliamua kusimamisha shilingi kuhusu hatima yake ndani ya timu hiyo, upande wakihisi atatoboa huku upande mwingine wa hisia zao ukiona anaweza kuchemsha.
Hata hapa kijiweni hatukuwa na imani kubwa na Nabi na tuliamua kujituliza kwanza tuone nini atakifanya ndani ya Yanga kuliko kujimaliza mapema kwa kumtabiria mazuri au mabaya halafu baadaye tukaja kuumbuka.
Alichokifanya Nabi kikatuweka midomo wazi na kikampa umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kwani aliipa Yanga mataji ya ligi na mengine ya ndani huku akiifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilipoteza kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria baada ya sare ya mabao 2-2 katika mechi mbili baina yao.
Alipotoka Yanga akaenda Morocco akaiimarisha FAR Rabat ikawa tishio na ilikaribia kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya huko, hivyo jina lake likazidi kuwa kubwa na maarufu Afrika hadi kupelekea Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kumnyakua ikiamini ataiwezesha kurudisha heshima yake.
Lakini mambo yanaonekana kumuendea kinyume Nabi ndani ya Afrika Kusini kutokana na mwenendo usioridhisha wa Kaizer Chiefs ambayo muda huu unaposoma andiko hili, inashika naafsi ya saba kwenye msimamo wa ligi kuu Afrika Kusini ikiwa na pointi 15 huku kinara Mamelodi Sundowns ikiwa na pointi 30.
Labda Kaizer Chiefs ina matatizo mengi nyuma ambayo yanachangia ifanye vibaya lakini kiuhalisia inampitisha Nabi katika njia ya miba ambayo akifanikiwa kuivuka atajenga heshima kubwa lakini kinyume na hapo itashusha hadhi na wasifu wake.
Akivumiliwa anaweza kutoboa lakini wale Kaizer Chiefs sidhani kama wanaweza kuwa na uvumilivu huo.