Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mtuhumiwa Masanja Mihayo, Miaka 31, Mkulima, Mkazi wa Ikandilo Wilaya ya Geita kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake aitwaye Mihayo Masanja, Miaka 10 kisha kuuzika mwili wake kwenye shamba la Mahindi na Pamba.
Tukio hilo limetokea mwezi Oktoba 2024 ndani ya Hifadhi ya Pori la Serikali Kata ya Nyaruyeye Tarafa ya Busanda Wilaya ya Geita na baadaye kubainika Januari 09, 2025 baada ya Mama mzazi wa watoto hao kuhitaji kuwaona watoto wake bila mafanikio;
Mama huyo alipokosa ushirikiano kutoka kwa mzazi mwenzake alitoa taarifa Polisi na Masanja Mihayo alipokamatwa na kuhojiwa alikiri kumuua mtoto wake na kuwapeleka Askari Polisi mahali alipouzika mwili huo ambapo taratibu za kisheria za kufukua mwili zilifanyika.
Imebainika kuwa marehemu Mihayo Masanja alishambuliwa kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia kipande cha mti wakati akiadhibiwa na baba yake mzazi na kupelekea kuvimba mwili wote; Baba mzazi alipoamka asubuhi alikuta mtoto huyo amefariki na kuamua kuuzika mwili huo kwenye shamba la Mahindi na Pamba.
Ni kwamba, kabla ya tukio la mauaji mwezi huo huo wa Oktoba 2024 marehemu na mdogo wake mwenye Miaka 09 (jina linahifadhiwa) waliondoka ndani ya Hifadhi ya Pori hilo ili waende Katoro kwa Mama yao mzazi aitwaye Joyce Andrew lakini hawakufanikiwa kwani Baba yao aliwarejesha. Kutokana na tabia hiyo, mtuhumiwa alichukizwa na kitendo cha watoto hao kutoroka na kwenda kwa Mama yao hivyo aliamua kumuadhibu Mihayo Masanja ambaye ni mtoto mkubwa ili asirudie tabia hiyo.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za uchunguzi wa kisayansi tunaendelea kukamilisha uchunguzi kwa kuzingatia taratibu za kisheria na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilisha taratibu za kisheria na uchunguzi wa kisayansi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linaendelea kuwaasa wananchi kuwa na utii wa sheria bila shuruti na kuwataka kuacha mara moja tabia ya kujichukukia Sheria mkononi.