YANGA imekuwa ikitajwa kutaka kumtema mshambiliaji Jean Baleke, lakini inaelezwa hadi sasa mambo bado magumu kutokana na kuwepo kwa vipengele vinavyoufanya mkataba baina yao usivunjike kirahisi.
Awali, Yanga ilitaka kumpeleka Baleke kwa mkopo Namungo, lakini mchezaji anataka mkataba uvunjike alipwe chake na maisha mengine yaendelee, hivyo wanaendelea kujadiliana kuona jambo hilo wanalimaliza kwa uharaka.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka Yanga, kwamba kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic alimuita mezani Baleke na kumueleza hayupo katika mipango yake, hivyo atafute timu ili kuendelea kukilinda kiwango chake.
“Hata hivyo, Baleke anataka mkataba uvunjike na sio kupelekwa kwa mkopo, kuna vipengele ndani ya mkataba wake ambavyo lazima vijadiliwe kuona jambo hilo linamalizika kwa amani,” kilisema chanzo hicho.
Mwanaspoti liliamua kumsaka Baleke ambaye ilielezwa awali alishapewa barua ya ‘thank you’ ili atafute mahali pengine kwa kuendeleza kipaji chake na mchezaji huyo alikiri kuwepo kwa mazungumzo ya kuvunja mkataba ila hakuwa tayari kulizungumza kwa kina.
“Siwezi kuzungumza nini kinaendelea kwa kina, ila kila kitu kikikaa sawa viongozi wa Yanga watazungumza na mimi nitazungumza, labda uniulize ligi ya msimu huu umeionaje nitakujibu ni nzuri licha ya mimi kutopata nafasi ya kucheza,” alisema Baleke aliyetua Yanga msimu huu akitokea Al-Ittihad ya Saudi Arabia alikokuwa akiicheza kwa miezi sita baada ya kuachana na Simba.